Putin, Kim watia saini makubaliano ya ushirikiano
19 Juni 2024Hatua hiyo inadhamiria kutanua ushirikiano wa kiuchumi na kijeshi na kuwa nguvu moja dhidi ya Marekani.
Shirika la habari la TASS liliripoti kuwa Putin alisema kuwa wamejadili masuala ya usalama na ajenda ya dunia.
Putrin aliongeza kwamba makubaliano hayo, yaliyotiwa saini baina ya mataifa hayo mawili, yanatoa nafasi ya kusaidiana endapo nchi zao zitakabiliwa na uchokozi.
Soma zaidi: Urusi na Iran kutia saini mkataba mpya wa ushirikiano hivi karibuni
Vyombo vya habari vya Urusi vilisema Putin na Kim walizungumza ana kwa ana kwa karibu masaa mawili katika mkutano ambao ulikuwa umepangiwa kudumu kwa saa moja tu.
Ziara ya Putin nchini Korea Kaskazini inafanyika wakati ambapo kuna hofu kuhusiana na mpango wa silaha ambapo Korea Kaskazini inaipa Urusi silaha inazozihitaji pakubwa kwa ajili ya vita vyake nchini Ukraine, ili nayo Urusi iisaidie Korea kaskazini kwenye teknolojia.