Putin azuru Mongolia akaidi kibali cha kukamatwa kwake
3 Septemba 2024Safari ya Putin ni ya kwanza kwa nchi mwanachama wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai tangu ilipotolewa hati hiyo ya kumkamata takriban miezi 18 iliyopita.
Kabla ya ziara yake, Ukraine iliitaka Mongolia imkamate Putin na kumkabidhi kwenye Mahakama ya mjini The Hague. Msemaji wa rais Putin alisema wiki iliyopita kwamba Urusi haina wasiwasi.
Soma pia: Putin asifu kasi ya vikosi vyake dhidi ya Ukraine
Hati hiyo inaiweka serikali ya Mongolia katika wakati mgumu.
Nchi wanachama wa ICC na zinazofungamana na mkataba wa Roma zinatakiwa zitekeleze sheria ya kuwaweka kizuizini washukiwa ikiwa hati ya kuwakamata imetolewa lakini Mongolia, nchi isiyo na bandari, inayopakana na Urusi inamtegemea sana jirani yake huyo kwa mafuta na umeme wake.
Umoja wa Ulaya umeonyesha wasiwasi kwamba Mongolia inaweza isitekeleze amri hiyo. Wakati huo huo Mahakama ya ICC haina utaratibu unaohakikisha kwamba hatua zake zinatekelezwa.