Putin azishutumu Ukraine, Magharibi kuchochea mauaji Urusi
27 Juni 2023Katika hotuba yake ya kwanza tangu kulipozuka uasi huo siku ya Jumamosi, Putin alisema alitoa agizo la moja kwa moja la kuepusha umwagikaji mkubwa wa damu na kutoa kinga kwa wapiganaji wa Wagner, ambao uasi wao ulitoa changamoto kubwa zaidi katika utawala wake wa miongo miwili.
Putin alieleza kuwa wapiganaji wa Wagner wanaweza kuchagua kujiunga na jeshi la Urusi, kuelekea Belarus au hata kurudi makwao.
Soma zaidi: Yevgeny Prigozhin aeleza sababu za kufanya uasi
Hapo awali, kiongozi wa kundi la mamluki la Wagner, Yevgeny Prigozhin, naye alivunja ukimya baada ya kutoa tamko kwa mara ya kwanza tangu uasi wa Jumamosi kupitia mkanda wa sauti uliosambazwa kwenye mtandao wa Telegram.
Kiongozi huyo alidai hakuwa na dhamira ya kupindua serikali ya Moscow bali alilazimika kufanya uasi kujibu mashambulizi dhidi ya wapiganaji wake.
Hadi sasa Prigozhin hafahamiki alipo ingawa alieleza Jumamosi kwamba angelielekea Belarus.