Putin asema yuko tayari kwa majadiliano kuhusu Ukraine
25 Desemba 2022Akizungumza kupitia mahojiano na kituo cha televisheni cha Rossiya 1 siku ya Jumapili (Disemba 25), rais wa Urusi, Vladmir Putin alisema bado ipo fursa ya kulizungumza na kulimaliza suala la Ukraine ikiwa kila upande una dhamira hiyo.
"Tupo tayari kwa majadiliano na yeyote anayejihusisha na mgogoro huu juu a suluhisho linalokubalika, lakini hilo ni juu yao - sisi sio tunaokataa kuzungumza, ni wao." Alisema kiongozi huyo wa Urusi.
Uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine tarehe 24 Februari umechochea mzozo mkubwa kabisa kuwahi kujiri barani Ulaya tangu Vita va Pili vya Dunia na makabiliano makubwa kati ya Moscow na Magharibi tangu Mzozo wa Makombora wa Cuba mwaka 1962.
Tangu wakati huo, kumekuwa na hatua chache za kukomesha vita hivi vya miezi kumi sasa nchini Ukraine, huku Kremlin ikisema itapambana hadi malengo yake yatimie na Kyivikisema haitakaa kitako hadi kila mwanajeshi wa Urusi aondolewe kwenye mamlaka yake, ikiwemo Crimea iliyotwaliwa na Urusi mwaka 2014.
"Magharibi ilitaka kuigawa Urusi"
Lakini Putin alikiambia kituo hicho cha televisheni kwamba nchi yake inapigana vita vya kujilinda. "Naamini kwamba tupo kwenye muelekeo sahihi, tunalinda maslahi yetu kama taifa, maslahi ya raia wetu, watu wetu. Na hatuna chaguo jengine zaidi ya kuwalinda raia wetu." Alisema akiongeza kwamba Ukraine na mataifa ya Magharibi yakiongozwa na Marekani, yalikuwa yanajaribu kuisambaratisha Urusi.
"Katikati ya yote haya ni sera ya wapinzani wetu kwenye siasa za kilimwengu wanaodhamiria kuirarua Urusi, ile Urusi ya kihistoria. Siku zote wamekuwa wakijaribu kutumia sera ya 'wagawe uwatawale'... Lengo letu ni kitu chengine: kuwaunganisha watu wa Urusi." Alisema.
Kuhusiana na msaada wa mifumo ya ulinzi ya Patriot ambayo Marekani imeipatia Ukraine, Putin alisema ana uhakika wa asilimia 100 kwamba vikosi vyake vitaiharibu mifumo hiyo.