Putin asema malengo yake Ukraine yatafanikiwa
12 Aprili 2022Akizungumza wakati akitembelea kituo cha kurushia vyombo vya anga za juu mashariki mwa nchi yake siku ya Jumanne (Aprili 12), Putinalirejelea kauli yake kwamba Ukraine ilikuwa imegeuzwa kichwa-ngumu dhidi ya Urusi, ambapo makundi ya siasa kali za kizalendo na wanazi mamboleo yalikuwa yanakuzwa.
Akiwa na mgeni wake, Rais Alexander Lukashenko wa Belarus, kwenye kituo hicho cha Vostochny, Putin alisema kwamba "operesheni maalum ya Urusi" ilikuwa na lengo la kuwalinda watu wa maeneo ya mashariki mwa Ukraine yanayodhibitiwa na waasi wanaoungwa mkono na Urusi na pia "kuhakikisha usalama wa Urusi," akiongeza kwamba malengo hayo yatatimia.
Putin, ambaye hiyo ilikuwa ziara yake ya kwanza nje ya mji mkuu Moscow, tangu kuanza kwa uvamizi wa nchi yake, aliapa kuwa Urusi haiwezi kutengwa na yenyewe haina lengo la kujitenga na ulimwengu.
Alitumia ziara hiyo kuyaonya mataifa yanayoiwekea vikwazo Urusi kwamba athari za vikwazo hivyo zitayarejea wenyewe.
WTO yatabiri kushuka kwa biashara ulimwenguni
Wakati huo huo, Shirika la Biashara Duniani (WTO) lilisema "biashara ya bidhaa itashuka kuliko ilivyotazamiwa awali mwaka huu" kutokana na vita vya Urusi nchini Ukraine.
Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Ngozi Okonjo-Iweala, aliielezea hali ya kibiashara duniani kuwa imepata mapigo mawili yaliyofuatana: kwanza virusi vya corona na sasa vita nchini Ukraine.
Awali, WTO ilikuwa imetabiri kwamba biashara ingelipanda kwa asilimia 4.7, lakini kutokana na vita hivyo, sasa imeshusha makadirio hayo na kuwa asilimia 3 tu.
Uhalifu wa kivita?
Kwenyewe nchini Ukraine, mamlaka zilisema zimeanzisha uchunguzi wa uhalifu wa kivita baada ya mzee wa miaka 64 kuuawa na bomu la kutegwa ardhini kwenye eneo ambalo wanajeshi wa Urusi wamejiondowa hivi karibuni.
Polisi ilisema mwanamme huyo alikuwa akiendesha gari yake katika kijiji cha Krasne kaskazini mwaUkraine na alikuwa ameshuka kuwasalimia jamaa, alipokanyaga bomu na kufa hapo hapo.
Mamlaka nchini humo zimekuwa zikiwaonya raia kwamba kuna mabomu ya kutegwa ardhini na mitego ya miripuko kwenye maeneo ambayo wanajeshi wa Urusi walikuwapo.
Wakimbizi wapindukia 330,000 Ujerumani
Serikali ya Ujerumani ilisema hadi Aprili 12 ilishawapokea wakimbizi zaidi ya 330,000 kutoka Ukraine.
Wizara ya Mambo ya Ndani ilisema polisi imewasajili watu 335,578 walioingia tangu uvamizi wa Urusi kuanza mnamo tarehe 24 Februari, ambapo wengi wao ni watoto na wanawake.
Lakini idadi kamili ya wakimbizi waliopo Ujerumani inaweza kuwa kubwa zaidi, kwani hakuna udhibiti mkubwa kwenye mpaka wake wa mashariki na raia wa Ukraine wanaweza kukaa kwenye Umoja wa Ulaya hadi siku 90 bila ya kibali.
Maafisa wanasema idadi nyengine kubwa pia ya wakimbizi hao wameshakwenda kwenye mataifa mengine ya Ulaya.