Prince Harry ajivunia ushindi dhidi ya Magazeti ya Murdoch
22 Januari 2025Prince Harry ametangaza ushindi wa "kihistoria" dhidi ya kundi la magazeti ya Rupert Murdoch nchini Uingereza baada ya kufikiwa kwa makubaliano muhimu katika kesi yake dhidi ya News Group Newspapers (NGN). Kwa mara ya kwanza, mchapishaji huyo alikubali matendo haramu ya The Sun na kukubali kulipa fidia kubwa.
Duke wa Sussex, mwenye umri wa miaka 40, aliishtaki NGN - inayochapishaji magazeti ya The Sun na News of the World (ambayo sasa haipo) - akidai ukusanyaji haramu wa taarifa binafsi kati ya mwaka 1996 na 2011.
Kesi hiyo pia ilihusisha uingiliaji wa faragha ya mama yake mzazi, Princess Diana. Vyanzo vilithibitisha kuwa makubaliano hayo yalizidi pauni milioni 10, zikiwa ni gharama kubwa za kisheria.
Kukiri Matendo Haramu
Katika taarifa ya pamoja na mlalamikaji mwenzake Tom Watson, Harry alisema: "Katika ushindi wa kihistoria leo, News UK imekiri kuwa The Sun, gazeti kuu la vyombo vya habari vya Rupert Murdoch nchini Uingereza, limejihusisha na vitendo vya kihalifu. Leo, uongo umeanikwa. Leo, kuficha ukweli kumefichuliwa. Na leo, imethibitishwa kuwa hakuna aliye juu ya sheria. Wakati wa uwajibikaji umefika."
Soma pia:Filamu ya maisha ya Harry na Meghan yawapa kiwewe waingereza
Taarifa hii ilisomwa na wakili David Sherborne nje ya Mahakama Kuu ya London, ambako kesi hiyo ilipangwa kuanza. Majadiliano ya dakika za mwisho yalipelekea NGN kuomba msamaha kamili kwa matendo yao.
Sherborne alibainisha kuwa NGN ilikiri uvamizi mkubwa wa faragha ya Harry na ya Princess Diana wakati wa miaka yake ya ujana. Mchapishaji huyo pia alikubali kumlenga Watson, mwanasiasa wa zamani wa Uingereza, alipokuwa waziri mdogo chini ya Waziri Mkuu wa wakati huo, Gordon Brown.
Ingawa NGN iliomba msamaha kwa matendo ya wapelelezi wa kibinafsi walioajiriwa na The Sun, ilisisitiza kuwa waandishi wa gazeti hilo hawakuhusika. "Kuna udhibiti na taratibu madhubuti katika machapisho yetu yote kuhakikisha kuwa hayawezi kutokea tena," alisema msemaji wa NGN.
Wigo wa kashfa
NGN imekumbana na zaidi ya kesi 1,300 zinazohusiana na udukuzi wa simu na shughuli nyingine haramu, zikiwa zimeigharimu zaidi ya pauni bilioni moja. Awali, NGN ilikanusha madai yoyote ya makosa yaliyofanywa na The Sun au watendaji wake wakuu.
Soma pia: Meghan Markle aungwa mkono kuibuwa ubaguzi kwenye Ufalme wa Uingereza
Kesi ya Harry ililenga kuwawajibisha watu hawa, hasa Rebekah Brooks, aliyekuwa mhariri wa The Sun na sasa Mkurugenzi Mtendaji wa News UK. Hata hivyo, makubaliano hayo hayakutaja makosa yoyote ya watendaji wa ngazi za juu wala kushughulikia tuhuma za kuficha ukweli.
Tom Watson alimtaka Rupert Murdoch kuomba msamaha kwa Harry na Mfalme Charles, akisisitiza haja ya uwajibikaji wa jumla. Wakati huohuo, Prince William, kaka yake Harry, alimaliza kesi kama hiyo na NGN mwaka 2020 kwa fidia ya "kiasi kikubwa," kulingana na timu ya kisheria ya Harry.
Ingawa NGN inadai kuwa makubaliano haya yanaweza kufunga mlango wa kesi nyingine za aina hii, Harry na Watson wameomba uchunguzi zaidi juu ya madai ya kiapo cha uongo na kuficha ukweli kwa taasisi hiyo.
Kesi hii imeibua upya mjadala wa maadili ya vyombo vya habari na uwajibikaji wa wachapishaji wakubwa. Wakati polisi mjini London ikisubiri mawasiliano zaidi, kashfa hii inaonyesha athari za kudumu za vitendo haramu vya vyombo vya habari kwenye imani ya umma.