Presseschau: Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani
21 Septemba 2017Maoni ya mhariri wa gazeti la Lausitzer Rundschau juu ya kauli iliyotolewa na mkuu wa wafanyakazi katika ofisi ya kansela Peter Altmier wa chama cha CDU akiwaambia watu bora kuacha kupiga kura kuliko kukichagua chama cha AfD cha mrengo mkali wa kulia kinachowapinga wahamiaji. Mhariri huyo anasema kauli ya mkuu huyo wa utumishi sio ya busara kwa sababu chama hicho cha mrengo mkali wa kulia kinaweza kupata mtaji wa kisiasa kwa kujionyesha kuwa kinaonewa na hivyo kuwafanya wapiga kura kuviadhibu vyama vingine kwa kuvinyima kura. Mhariri wa gazeti la Handels Blatt anasema kauli ya bwana Peter Altmier inakiuka maadili kwa sababu kupiga kura ni haki kuu ya kila mtu katika demokrasia.
Na maoni ya Rheinische Post juu ya Uhispania ambako polisi wa nchi hiyo wametwaa mamilioni ya karatasi za kupigia kura ya maoni juu ya kujitenga kwa jimbo la Catalonia. Mhariri anasema serikali ya Uhispania inaamini kwamba harakati za jimbo la Catalonia za kutaka kujitenga zinakiuka katiba lakini serikali hiyo ingeliweza kuzizuia juhudi hizo mapema endapo bunge la taifa lingeliruhusu kufanyika kwa kura ya maoni katika jimbo hilo. Ungelikuwapo uwezekano mkubwa kwa watu kuchagua kuendelea kuwamo katika umoja wa Uhispania.
Naye mhariri wa gazeti la Süddeutsche Zeitung anatoa mwito kwa Umoja wa Ulaya kujaribu kuingilia kati swala hilo la Uhispania ingawa kisheria Umoja huo hauna uwezo wa kufanya hivyo mhariri anaeleza kwamba viongozi wa Umoja wa Ulaya wanapaswa kumshauri waziri mkuu wa Uhispania Mariano Rajoy ajaribu kuwapa watu wa jimbo la Catalonia chochote. Uhispania inaweza kuuepuka mgogoro huo ikiwa serikali kuu itaacha kuwaandama wanasiasa wa jimbo la Catalonia ambao wanatumia haki ya kidemokrasia kama vile ilivyotokea Uingereza na Scottland.
Na kuhusu maoni juu ya tabia ya kuchora michoro yenye kuwakejeli Wayahudi kwenye makaburi au majengo yao mhariri wa gazeti la Die Welt anasema polisi wa Ujerumani wanaizingatia tabia hiyo kuwa ni uhalifu wa kawaida tu lakini hilo ni swala la kisiasa na gazeti la Badische Zeitung linasema haitoshi tu kusema tabia hiyo ni chuki dhidi ya Wayahudi bali hilo ni swala linalo hitaji msimamo wa kisiasa.
Mwandishi:Zainab Aziz/dpa/inlandspresse
Mhariri:Josephat Charo