Pongezi zamiminika baada ya makubaliano ya CDU/CSU na SPD
8 Februari 2018Rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Juncker ameyakaribisha makubaliano ya kuunda serikali ya mseto nchini Ujerumani kati ya vyama vya kihafidhina vya CDU/CSU na kile cha Social Democratic SPD. Bwana Juncker amesema anaikaribisha hatua ya serikali mpya ya Ujerumani kuhusiana na dhamira iliyonayo katika masuala ya sera za Umoja wa Ulaya.
Martin Selmayr mkuu wa watumishi kwenye ofisi ya Juncker, ameyapokea kwa furaha makubaliano hayo yaliyo kwenye mkataba wenye kurasa 170 utakaofanya kazi kwa miaka minne, mkataba huo mwanzoni mwake tu unaanza na sura inayosisitiza Ulaya yenye nguvu, pamoja na nukuu nyingi za mfumo wa Umoja wa Ulaya katika sekta zote.
Rais wa zamani wa Bunge la Ulaya Martin Schulz, ambaye ni mwenyekiti wa sasa wa chama cha Social Democratic (SPD) anayetarajiwa kuchua wadhfa wa Waziri wa Mambo ya nje wa Ujerumani katika serikali mpya, amepongeza makubaliano hayo ya kuunda serikali yaliyofikiwa hapo jana Jumatano pamoja na kansela wa Ujerumani Angela Merkel. Schulz amesema hiyo ina maana kwamba Ujerumani sasa itarejea kwenye jukumu lake kama kiongozi wa Umoja wa Ulaya. Bwana Schulz amesema jambo muhimu ni kwamba serikali iko tayari kuongeza zaidi katika bajeti ya Umoja wa Ulaya. Amefahamisha kuwa mara nyingi amezungumza na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kwa njia ya simu na kwamba anataka kufanya kazi pamoja na Ufaransa ili kufanikisha kuwepo na "Ulaya iliyo bora zaidi na inayozingatia haki."
Kansela Angela Merkel amesema makubalaino hayo yatawezesha kuundwa kwa serikali imara kama inavyotarajiwa na ulimwengu mzima. Kamishna wa Uchumi wa Umoja wa Ulaya Pierre Moscovici baada ya kulipokea tangazo hilo aliandika kupitia kwenye ukurasa wake wa Twitter: "Mkataba uliofikiwa wa muungano wa vyama vya Ujerumani ni habari njema hata kwa Ulaya!"
Wakati huo huo matumizi ya Serikali yanatarajiwa kuongezeka kwa ajili ya elimu na ujenzi wa miundombinu hapa nchini Ujerumani, katika wizara ya fedha itakayoongozwa na Waziri mpya Olaf Scholz, ambaye kwa sasa ni Meya wa jiji bandari la Hamburg lililopo kaskazini mwa Ujerumani. Uteuzi huu muhimu ni baada ya miaka ya kubana matumizi na udhibiti mkubwa wa matumizi chini ya waziri wa zamani wa fedha Wolfgang Schäuble.
Mwandishi:Zainab Aziz/p.dw.com/p/2sHhA
Mhariri: Iddi Ssessanga