1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pompeo: Marekani itaendelea kuipa kipaumbele Israel

24 Agosti 2020

Marekani inasema itahakikisha Israel inaendelea kuwa na kipaumbele cha kijeshi kwenye Mashariki ya Kati katika mikataba yoyote ya silaha ambayo Marekani itaingia na Umoja wa Falme za Kiarabu.

https://p.dw.com/p/3hQgp
Israel | PK US-Außenminister Mike Pompeo
Picha: picture-alliance/AP Photo/D. Hill

Pompeo aliyasema hayo siku ya Jumatatu (Agosti 24) akiwa kwenye kituo cha kwanza cha ziara yake ya eneo la Mashariki ya Kati kushinikiza muafaka kati ya Waarabu na Waisraeli, baada ya Agosti 13 nchi yake kufanikiwa kuanzishwa kwa mahusiano rasmi ya kibalozi baina ya Israel na Umoja wa Falme za Kiarabu. 

Akizungumza mbele ya waandishi wa habari akiwa na mwenyeji wake, Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu mjini Jerusalem hivi leo, Pompeo alisema ni kwa faida yao wenyewe, pale mataifa mengine ya Kiarabu yatakapoiona fursa ya kurejesha mahusiano mema na jirani yao Israel.

"Wakati nikitembelea mataifa mengine kwenye ziara hii, matumaini yangu ni kwamba tutayashuhudia mataifa mengine ya Kiarabu yakiungana kwenye hili. Hii ni fursa kwao ya kushirikiana kuitambua Israel ambayo sio tu itaimarisha utulivu Mashariki ya Kati, bali pia maisha ya watu wao." Alisema Pompeo, ambaye ziara yake ilitazamiwa kumfikisha pia Sudan, Umoja wa Falme za Kiarabu na Bahrain.

Israel yapewa kipaumbele

Israel Benjamin Netanjahu
Benjamin Netanyahu: Tumehakikishiwa uungwaji mkono wa Marekani.Picha: picture-alliance/Newscom/UPI PHoto/A. Sultan

Kuhusiana na suala la silaha na nguvu za kijeshi, Pompeo alisema licha ya kwamba wana mahusiano ya zaidi ya miaka 20 na Umoja wa Falme za Kiarabu kwenye mambo ya ulinzi na kwamba bado wanadhamiria kuendelea kulipatia taifa hilo la Ghuba silaha za kutosha kukabiliana na vitisho vya Iran, bado Marekani itaendelea kuipa Israel kipaumbele cha kiusalama.

Licha ya Marekani kufanikisha makubaliano hayo kati ya Israel na Umoja wa Falme za Kiarabu, nchini Israel kuna upinzani dhidi ya hatua ya Marekani kulipatia taifa hilo la Kiarabu silaha za kisasa kama vile ndege za kijeshi chapa F-35.

Netanyahu aliwaambia waandishi wa habari amehakikishiwa kwamba Marekani itaonesha uungaji mkono wake wa juhudi za amani baina ya Israel na Waarabu na kuunda mshikamano dhidi ya Iran.

Utawala wa Trump unayachukulia makubaliano kati ya Umoja wa Falme za Kiarabu na Israel kuwa ni alama kubwa ya kihistoria kwenye siasa zake za nje, katika wakati huu Trump akiwania kuchaguliwa tena katika uchaguzi wa Novemba mwaka huu. 

Hata hivyo, makubaliano hayo yamekosolewa vikali, huku Umoja wa Falme za Kiarabu ukitajwa kama msaliti wa mapambano ya Wapalestina.

Mpatanishi mkuu wa Wapalestina, Saeeb Erakat, ameuonya utawala wa Trump dhidi ya hatua yoyote ya kuwatenga wao kwenye juhudi za kidiplomasia za Mashariki ya Kati.