Pompeo kuhojiwa na Maseneta Marekani
25 Julai 2018Maseneta nchini Marekani wanaoonekana kuumizwa na tabia ya hivi karibuni ya bilionea huyo wa chama cha Republican watahitaji kupata majibu hii leo Jumatano kutoka kwa waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo wakati atakapowasilisha taarifa ya utendaji wake wa kazi akiwa ni mwanadiplomasia wa ngazi ya juu wa nchi hiyo ikiwa ni kipindi kifupi tangu ashike wadgifa huo.
Hayo yanajiri wakati wa bunge nchini Marekani wakiwa na shauku ya kufahamu kutoka kwa Pompeo juu ya mkutano muhimu wa kilele kati ya rais Donald Trump na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un uliofanyika Juni 12 nchini Singapore.
Shauku ya wabunge hao imeongezeka na kuonekana kuwa suala la haraka na muhimu zaidi baada ya mkutano wa Helsinki, hususani kikao cha pamoja kati ya viongozi hao wawili na waandishi wa habari ambapo Trump alionekana kwa wabunge wa chama chake cha Republican na wale wa Democrat kusaliti masilahi ya Marekani na kuonekana kukubaliana na Putin.
" Mkutano na waandishi wa habari wa Helsinki ulikuwa ni siku mbaya kwa nchi yetu na kila mtu anajua hilo" amesikika seneta Bob Corker, mwenyekiti wa kamati inayohusiana na mahusiano ya kimataifa wa chama cha Republican ambaye pia amekuwa akimkosoa mara kwa mara rais Donald Trump alipozungumza na waandshi wa habari.
Mkutano wa Helsinki kupewa kipaumbele
Suala la Urusi linatarajiwa kuchukua uzito wakati wa kikao kati ya Mike Pompeo na kamati ya bunge la Congress.
Hata hivyo Corker ameweka bayana kuwa kamati yake pamoja na mambo mengine itamuhoji pia waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo juu ya safari yake ya hivi karibuni nchini Korea Kaskazini, kauli ya rais Donald Trump dhidi ya NATO, Suala la ushirikiano wa pamoja katika masuala ya ulinzi, na msimamo wa Trump kuhusiana na viwango vipya vya kodi ambao sasa unaonekana kutaka kusababisha vita vya kibiashara.Pompeo amesema ataeleza mbele ya kamati hiyo juu ya masuala mengi likiwemo suala la uhusiano kati ya Marekani na Urusi na zaidi mkutano wa kilele kati ya Trump na rais Vladimir Putin wa Urusi.
Kikao hicho cha ndani kati ya Trump na Putin kimekosolewa na wabunge nchini Marekani lakini Pompeo amesisitiza kwamba mkutano huo umuhimu wake kwa dunia utaonekana hapo baadaye wakati historia itakapoandikwa.
Ikulu ya Marekani White House imetangaza kwamba rais wa Urusi Vladimir Putin amealikwa nchini Marekani kwa ajili ya mkutano mwingine baadaye mwaka huu mnamo wakati bunge la Congress likionekana kukerwa na yale yaliyojiri katika ziara ya Trump mjini Helsink hivi karibuni hasa alipoonekana kukubaliana na kauli ya Putin kukanusha kuingilia uchaguzi mkuu wa Marekani wa mwaka 2016 hatua iliyoonekana kupingana na uchunguzi wa mashirika ya kijasusi ya Marekani uliohitimisha Urusi iliingilia uchaguzi huo.
Kauli hiyo ya Trump mjini Helsinki ilisababisha mjadala mkubwa nchini Marekani kiasi ya kiongozi huyo kusema aliteleza ulimi na baaday kufafanua kuwa ana amini Urusi iliingilia uchaguzi huo.
Mwandishi: Isaac Gamba/ AFPE
Mhariri :Bruce Amani