1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pompeo awasili Riyadh kwa mazungumzo kumhusu Khashoggi

16 Oktoba 2018

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo amewasili mjini Riyadh huku kukiwa na ripoti katika vyombo vya habari Marekani zinazosema kwamba Saudi Arabia inajiandaa kusema Jamal Khashoggi aliuwawa wakati wa mahojiano.

https://p.dw.com/p/36bRI
Malaysia Mike Pompeo
Picha: Getty Images/AFP/M. Vatsyayana

Rais wa Marekani Donald Trump alimuamuru Pompeo asafiri kuelekea Saudi Arabia Jumatatu baada ya kuzungumza na Mflame Salman kwa njia ya simu.

Rais Trump amesema wauwaji ndio waliohusika katika kupotea kwa Khashoggi na akasema mfalme huyo amekanusha kabisa kuhusika kwa namna yoyote. Uturuki ambako Khashoggi alipotelea tarehe 2 ya mwezi huu baada ya kuingia katika ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul, imesema inaamini aliuwawa ndani ya jengo hilo, madai ambayo Saudi Arabia imekuwa ikiyakanusha.

CNN imetaja vyanzo kadhaa ikisema Saudi inataka kubadilisha karata

Usiku wa Jumatatu gazeti la New York Times na shirika la habari la CNN viliripoti kwamba Saudi Arabia inaandaa maelezo tofauti yaliyo na lengo la kuzima mzozo wa kisiasa waliouanzisha. Lakini Rais Trump anasema hakuna anayejua kama ripoti hizo za vyombo vya habari ni rasmi.

Türkei Polizeiforensik-Experten treffen im saudi-arabischen Konsulat in Istanbul ein
Maafisa wa ujasusi wa Uturuki waingia ubalozi wa Saudi Arabia IstanbulPicha: Reuters/M. Sezer

"Tunafanya kazi pamoja na Saudi Arabia na Uturuki na wanafanya kazi pamoja kubaini kilichotokea. Na wanataka kujua kilichotokea pia, kwa hiyo watu wengi wanalifanyia kazi jambo hilo, tutaona itakavyokuwa. Nimesikia kuhusu hiyo ripoti ila hakuna ajuaye kama ni ripoti rasmi. Kwa sasa ni uvumi tu, ni uvumi wa ripoti iliyotoka," alisema Trump.

Ikitaja vyanzo kadhaa CNN imesema kwamba Saudi Arabia inapanga kusema kwamba Khashoggi aliuwawa wakati wa mahojiano ambayo yalikuwa yanalenga kupelekea kutekwa nyara kwake. Nalo gazeti la New York Times likinukuu chanzo kilicho karibu na mipango ya Saudi Arabia, limesema nchi hiyo ya kifalme inapanga kusema kuwa mwanahabari huyo aliuwawa na afisa wa kijasusi aliyekuwa na hamaki na ambaye alitaka kulificha tukio hilo.

Madai hayo yataonekana kukinzana na taarifa iliyotolewa na maafisa wa Uturuki ambao wamesema maafisa 15 wa kijasusi wa Saudi Arabia akiwemo mtaalam wa upasuaji waliingia na kutoka mjini Istanbul siku ambayo Khashoggi aliuwawa.

Umoja wa Ulaya unataka uchunguzi uwe wenye uwazi

Huku hayo yakiarifiwa kikosi cha wachunguzi wa Uturuki na Saudi Arabia kimeondoka katika ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul mapema Jumanne baada ya kufanya uchunguzi wa masaa tisa katika jengo hilo. Kulingana na shuhuda mmoja wa shirika la habari la Reuters, mwendesha mashtaka mmoja wa Uturuki aliondoka karibu saa moja na nusu baadae.

Federica Mogherini Hohe Vertreterin EU Aussenpolitik
Mwakilishi mkuu wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya Federica MogheriniPicha: Consilium/M. Salerno

Umoja wa Ulaya kupitia kwa mwakilishi wake mkuu wa mambo ya nje Federica Mogherini umetaka kuwepo na uwazi katika uchunguzi huo .

"Tumekubaliana na kila mmoja kwamba tunatarajia uwazi, uwazi katika uchunguzi huo utakaofanywa na Saudi Arabia kwa ushirikiano na Uturuki. Nafikiri tuko katika ukurasa mmoja na rafiki zetu wa Marekani katika hili," alisema Mogherini.

Ushahidi ambao umechukuliwa na wachunguzi wa Uturuki katika ubalozi huo haujulikani kwa kuwa maafisa wa Saudia wamekuwa wakiingia na kutoka jengo hilo tangu kupotea kwa Khashoggi Oktoba 2 bila ya kuzuiliwa na yeyote.

Mwandishi: Jacob Safari/APE/DPAE/Reuters

Mhariri: Iddi Ssessanga