Pompeo atetea mkutano wa Trump na Putin
26 Julai 2018Hayo yanajiri huku maseneta kutoka vyama vya Republican na Democrats wakiendelea kumkosoa Trump hususani kwa matamshi yake ya hivi karibuni aliyoyatoa wakati wa mkutano wa kilele kati yake na rais Vladimir Putin wa Urusi ambapo alishindwa kumbana Putin juu ya madai ya kuingilia uchaguzi wa Marekani wa mwaka 2016 na kuonekana kukubaliana naye hatua iliyoibua mjadala nchini Marekani licha ya Trump kulazimika kufafanua baadaye kuwa aliteleza ulimi na hakumaanisha hivyo.
Rais Vladmir Putin amekuwa akikanusha Urusi kuingilia uchaguzi huo huku Trump naye akisema hakukuwa na makubaliano yoyote juu ya hilo kati ya Marekani na Urusi. Suala hilo kwa sasa liko chini ya kamati ya uchunguzi inayoongozwa na mwanasheria Robert Mueller.
Kamati hiyo ilizidi kumbana Mike Pompeo ikisisitiza kupata taarifa juu ya kipi kilichojadiliwa kati ya Trump na Putin wakati viongozi hao walipokuwa peke yao isipokuwa wakalimani kwa karibu masaa mawili.
Pompeo amesema aliaarifiwa kwa ufasaha kuhusiana na mkutano huo wa ana kwa ana kati ya Trump na rais wa Urusi Vladimir Putin ambaye mashirika ya kijasusi ya Marekani yanadai kuwa alifahamu juu ya hatua ya Urusi kuingilia uchaguzi wa Marekani mwaka 2016.
Huku akionekana kujikakamua kutoa ufafanuzi Pompeo alisisitiza kuwa rais ana haki ya kufanya mikutano ya faragha na kuongeza kuwa hata hivyo ana fahamu vema kuhusiana na kile kilichojadiliwa wakati huo na viongozi hao wawili.
Seneta Bob Corker mwenyekiti wa kamati hiyo ya mambo ya nje alimueleza Pompeo kuwa maseneta wana mashaka na utendaji kazi wa ikulu ya Marekani ikiwa ni pamoja na hatua zinazohusiana na sera za nje za Marekani.
Aliongeza kuwa mashaka hayo yanatokana na kauli za mara kwa mara zinazokanganya zinazotolewa na rais Donald Trump ikiwa ni pamoja na uchunguzi unaoendelea dhidi ya Urusi inayohusishwa na kuingilia uchaguzi wa Marekani mwaka 2016 na matamshi ambayo Trump amekuwa akiyaelekeza dhidi ya nchi washirika.
" Nina imani kubwa na wewe , nadhani wewe ni mzalendo isipokuwa tu matendo ya rais ndio yanaonekana kulifanya taifa letu lisiaminike" aliongeza Corker.
Aidha Corker alihoji juu ya kauli ya Trump kumsifia kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un kuwa ana kipaji kikubwa na anawapenda watu wake hasa ukichukulia ukiukaji mkubwa dhidi ya haki za binadamu unaofanyika Korea Kaskazini.
Maswali mengine mazito yakiwemo yanayohusu Korea Kaskazini, NATO na Iran nayo pia yaliulizwa na wajumbe wa kamati hiyo huku Pompeo akisema hapaswi kufichua maudhui ya mazunguzo hayo.
Mike Pompeo alifafanua kuwa baadhi ya matamshi ya rais Trump yanazaa matunda na kutaka utawala wa Marekani kuhukumiwa kwa matendo yake badala ya matamshi ya rais.
Kwa upande mwingine mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Marekani akizungmzia suala la Korea Kaskazini alisema safari ndefu bado ipo katika mchakato wa kuondoa silaha za nyukilia nchini Korea Kaskazini.
Mwandishi: Isaac Gamba /AFPE/EAP
Mhariri: Iddi Ssessanga