Polisi watawanya waandamanaji wa Kikurdi Kolon
28 Januari 2018Polisi imesema imewatawanya waandamanaji kutokana na kuwapo kwa mabango katika kundi la waandamanaji linaloonesha nembo ya chama cha wafanyakazi wa Kikurdi PKK , ambazo zimepigwa marufuku nchini Ujerumani.
Maandamano hayo yalitayarishwa na NAV-DEM , chama cha Wakurdi ambacho kinaelezwa kuwa karibu na chama kilichopigwa marufuku cha PKK, ambacho kimepigwa marufuku pia nchini Uturuki pamoja na washirika wake wa mataifa ya magharibi kuwa ni kundi la kigaidi.
"Idadi kubwa ya waandamanaji walishika mabango yenye picha ya kiongozi wa PKK aliyeko kifungongo Abdullah Ocalan," msemaji wa polisi mjini Kolon aliliambia shirika la habari la AFP.
Watu wawili walikamatwa katika maandamano hayo, ambayo yamekuja wiki moja baada ya vikosi maalum vya jeshi la Uturuki pamoja na waasi ambao ni washirika wa Uturuki nchini Syria kufanya mashambulizi wakiwalenga wanamgambo wa Kikurdi wa kundi la vikosi vya ulinzi wa umma YPG, kaskazini mwa Syria.
Hali ilishakuwa mbaya wakati maandamano hayo yalipoanza majira ya asubuhi katika mji huo wa magharibi mwa Ujerumani, ambapo zaidi ya polisi 2,000 walipowekwa kulinda maandamano hayo.
"Uhuru kwa Wakurdi" na "oneni aibu, Ulaya !" yameandikwa baadhi ya mabango waliyokuwa wamebeba waandanaji.
Polisi waliwazuwia waandamanaji karibu ya kufikia nusu ya safari yao kuhusiana na nembo za PKK na kuwasindikiza kuelekea walikoanzia.
Hakuna tukio baya lililotokea
Hakuna tukio lililoripotiwa mara moja, lakini "hali iliendelea kuwa tete," alisema msemaji wa polisi, na kuongeza kwamba alikuwa na wasi wasi juu ya mapambano kati ya waandamanaji na polisi , ama Waturuki wenye msimamo wa kizalendo , wakati giza litakapoingia.
Ujerumani wanaishi kiasi ya Wakurdi milioni moja na watu milioni 3 wenye asili ya Uturuki, na maafisa wameonya dhidi ya mivutano baina ya jamii hizo mbili.
Mapambano yalitokea kati ya watu kutoka makundi hayo mawili tangu pale Uturuki ilipoanzisha mashambulizi yake yaliyopewa jina la "tawi la mzaituni" ambapo misikiti mingi ya Waturuki nchini Ujerumani imekumbwa na matukio ya uharibifu.
"Uturuki imeanzisha vita vya kimabavu ambavyo vinavuka mipaka ya sheria za kimataifa," kiongozi mwenza wa jamii ya Wakurdi Mehmet Tanriverdi aliliambia gazeti la kanda la Heilbronner Stimme jana Jumamosi.
Mara nyingi wakielezwa kuwa ni idadi kubwa ya watu wasio na taifa , Wakurdi wamekuwa washirika muhimu katika mapambano dhidi ya kundi linalojiita Dola la Kiislamu, lakini baada ya mashambulizi ya hivi karibuni ya Uturuki wengi waliokuwa wakitafuta malipo wameachwa wakiwa wamevunjika moyo sana. Kumekuwa pia na maandamano madogo ya kuunga mkono Wakurdi nchini Ufaransa jana Jumamosi, ambapo mamia kadhaa ya watu waliandamana mjini Paris na karibu watu 500 waliandamana mjini Marseille.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / dpae
Mhariri: Isacc Gamba