1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Polisi waombwa kumkamata rais wa Korea Kusini

6 Januari 2025

Ofisi ya Kupambana na Ufisadi wa Maafisa wa Ngazi za Juu ya Korea Kusini imeliomba jeshi la polisi kuchukuwa jukumu la kumtia nguvuni rais aliyendolewa madarakani na bunge, Yoon Suk Yeol.

https://p.dw.com/p/4oqQU
Yoon Suk Yeol, Korea Kusini
Yoon Suk Yeol, rais wa Korea Kusini aliyeondolea madarakani na bunge.Picha: South Korean Presidential Office/Yonhap/AFP

Ombi hilo ni baada ya maafisa wake kushindwa kumuweka kizuizini kufuatia makabiliano ya masaa kadhaa na walinzi wa rais huyo wiki iliyopita.

Ofisi hiyo na jeshi la polisi zimethibitisha kuzungumzia suala hilo hivi leo, yakiwa yamebakia masaa machache kabla ya kumalizika kwa muda wa waranti wa wiki moja uliotolewa na mahakama.

Soma zaidi:Maelfu ya waandamanaji Korea Kusini wakusanyika Seoult 

Ofisi hiyo huenda ikaiomba mahakama kuipa waranti mpya wa kuongeza muda wa kumuweka Yoon kizuizini, kwa mujibu wa polisi. Mahakama ya Wilaya ya Seoul Magharibi ilikuwa imetowa waranti wa kumkamata Yoon mnamo tarehe 31 Disemba, baada ya kukwepa miito kadhaa ya kujitokeza kuhojiwa.

Ofisi ya kupambana na ufisadi inashirikiana na wapelelezi wa jeshi na polisi kuangalia endapo wafunguwe mashitaka ya uasi dhidi ya Rais Yoon, kufuatia amri yake ya kijeshi aliyoitowa Disemba 3 na kutuma wanajeshi kulizunguka jengo la bunge linalotawaliwa na vyama vya upinzani.