Polisi wamwagwa India kuwakabili wakulima wasiandamane
13 Februari 2024Vyombo vya habari vya ndani nchini India vimeonesha wingu zito la moshi wa mabomu ya machozi ukifuka baada ya polisi kuyafyetua walipokuwa wakiwakabili waandamanaji karibu na mji mdogo wa Ambala, umbali wa kiasi kilometa 200 kutoka New Delhi.
Polisi pia wameweka vizuzizi vya nyaya za chuma na zege kwenye njia zote kuu zinazozunguka majimbo matatu yanayokaribiana na mji mkuu.
Miongoni mwa madai mengine wakulima wa nchi hiyo wanaishinikiza serikali kuweka utaratibu wa kutangaza bei elekezi ya mazao. Wakulima nchini India wanayo nguvu kubwa kutokana na wingi wao unaofikia theluthi mbili ya idadi jumla ya watu bilioni 1.4 wa taifa hilo.
Mwaka 2021 walifanya maandamano yaliyoitikisa nchi hiyo na kuilazimisha serikali kubadili sheria kadhaa zilizozusha malalamiko.