Polisi wajaribu kudhibiti maadamano ya wanafunzi Bangladesh
6 Agosti 2018Wanafunzi kutoka shule za sekondari pamoja na vyuo wameandamana mjini Dhaka na maeneo mengine ya nchini humo huku wakiwasimamisha madereva na kufanya ukaguzi wa leseni zao na usajili wa nambari za magari yao.
Maandamano hayo ya wanafunzi yalioingia siku ya tisa siku ya Jumatatu (06.08.2018) yamesambaratisha usafiri katika maeneo mbali mbali nchini Bangladesh. Ni kawaida kwa watu kuendesha magari bila leseni halali nchini humo.
Wiki iliyopita maafisa kadhaa wa polisi na wa serikali walikutwa bila stakabadhi muhimu baada ya kutakiwa watoe hati hizo na waandamanaji. Kulingana na polisi watu takriban 3000 wanauwawa kila mwaka kutokana na ajali ya barabarani nchini Bangladesh huku shirika la usafiri binafsi nchini humo likisema watu takriban 7,397 waliuwawa mwaka uliopita kutokana na ajali hizo za barabarani.
Aidha maandamano hayo yanayoendelea kwa siku tisa sasa, saa nyengine yaligeuka na kuwa vurugu baada ya waandamanaji walio na ghadhabu kali kuyaharibu magari na kukabiliana na baadhi ya madereva.
Usafiri umerejeshwa baada ya kusitishwa kwa muda kufuatia hofu ya vurugu zaidi
Hata hivyo baadhi ya wafanyakazi katika sekta ya usafiri walianza tena kufanya kazi siku ya Jumatatu baada ya kuahirisha huduma zao kufuatia wasiwasi wa usalama wao na uwezekano wa magari yao kuharibiwa.
Mahbubur Rahman, Katibu wa mipango katika shirika la usafiri la Dhaka, amesema mabasi yanafanya kazi mjini na hata katika barabara za umbali mrefu.
Aidha polisi mjini humo imesema kwamba imewatia nguvuni watu watatu zaidi wanaodaiwa kujaribu kuanzisha vurugu kwa kusambaza habari zisizothibitishwa katika mitandao yao ya kijamii.
Mwishoni mwa juma lililopita polisi mjini Dhaka ilisema imewafungulia mashitaka ya uhalifu watumiaji 28 wa mitandao ya kijamii wa Facebook na Twitter kwa kueneza habari za uwongo juu ya maandamano yanayoendelea.
Hapo jana Jumapili jioni, polisi ilimzuwiya mpiga picha maarufu Shahidul Alam kufuatia maneno yake aliyoyaweka katika mtandao wake wa facebook juu ya maandamano hayo.
Mwandishi: Amina Abubakar/dpa
Mhariri: Daniel Gakuba