Polisi Brazil yasambaratisha kambi za wafuasi wa Bolsonaro
10 Januari 2023Mamia ya wanajeshi na polisi walitawanywa kwenye mji mkuu Brazilia kuzivunja kambi kadhaa za waandamanaji nje ya Makao Makuu ya jeshi la nchi hiyo.
Kwenye eneo hilo kulikuwa na kiasi wafuasi 3,000 wa rais wa zamani Jair Bolsonaro waliofunga mahema yaliyotumika kama kambi kwa maelfu ya waandamanaji walioyavamia majengo muhimu ya utawala mjini Brazilia siku ya Jumapili.
Operesheni hiyo imefanyika baada ya Mahakama ya Juu ya Brazil kutoa amri ya kuondolewa kambi zote za waandamanaji kufuatia uvamizi ulioyalenga majengo ya Bunge, Mahakama ya Juu na Ofisi rasmi ya rais wa nchi hiyo.
Polisi pia imesema imewakamata zaidi ya waandamanaji 1,500 wanaohusishwa na uvamizi huo ulioongozwa na wafuasi wa Bolsonaro ambao wanayapinga matokeo ya uchaguzi wa Oktoba iliyopita yaliyomnyima ushindi mwanasiasa huyo wa mrengo wa kulia.
Matokeo ya uchaguzi huo yalimwezesha mwanasiasa wa mrengo wa shoto Luiz Inacio Lula da Silva kuchaguliwa kuwa rais na aliapishwa zaidi ya wiki moja iliyopita.
Maandamano ya kulinda demokrasia yafanyika Sao Paulo
Katika hatua nyingine Mahakama ya Juu ya nchi hiyo imewondoa madarakani kwa muda wa siku 90 gavana wa jimbo la Brazilia Ibaneis Rocha.
Kiongozi huyo anayezingatiwa kuwa na usuhuba na Bolsonaro anatuhumiwa kutochukua hatua za kuimarisha usalama licha ya ishara zote za tahadhari zilizoonekana kabla ya uvamizi.
Tangu kutokea mkasa huo kumekuwa na ukosoaji mkubwa ndani na nje ya Brazil. Hapo jana mamia ya watu walikusanyika katikati mwaka mji wa Sao Paulo kwa maandamano ya kuilinda demokrasia na kushinikiza kuchukuliwa hatua kwa wote waliovamia majengo ya serikali siku ya Jumapili.
Waandamanaji ikiwemo vijana, watetezi wa haki za wafanyakazi na wanaharakati wanaopinga ubaguzi wa rangi waliteremka kwenye mitaa ya mji huo wakina mabango yaliyosomeka "Tuko pamoja na Lula na kwa ajili ya demokrasia" na mengine yakiwa na ujumbe unaosema "heshimu kura ya umma"
Fatima Lima Melo, ni mwanafunzi aliyeshiriki maandamano hayo amesema "Kile kinachoniumiza ni kutoadhibiwa kwa watu wanaotaka kuizika demokrasia ya nchi yetu, tuliyoipigania kwa nguvu kubwa. Demokrasia yetu ndiyo kwanza ina miaka 30 na ningependa ifikishe mamilioni ya miaka "
Lula arejea ofisini kwa ahadi ya kuwasaka walioshiriki uvamizi
Wakati hayo yakijiri, hapo jana jioni rais Lula alirejea ofisini kwake kwa mara ya kwanza tangu uvamizi wa mwishoni mwa juma.
Alifanya mkutano wa usalama na magavana 20 kwenye majengo ya ikulu mjini Brasilia na kisha akarudia ahadi yake ya kuwasaka wote waliohusika na vurumai ya Januari 8.
Baada ya mkutano huo picha za video zilimwonesha Lula akitembea kutoka ofisi za ikulu hadi kwenye viunga vya majengo ya Mahakama Kuu kujionea kwa mara nyingine uharibifu uliotokea.
Mapema kiongozi huyo alizungumza kwa njia ya simu na rais Joe Biden wa Marekani, ambako alipokea mwaliko rasmi wa kuitembelea Washington mnamo mwezi Februari.