Platini afikishwa mahakamani Uswisi kesi ya rushwa
15 Machi 2021Aliyekuwa rais wa shirikisho la kandanda Ulaya – UEFA Michel Platini atakuwa na siku tatu zenye shughuli nyingi mahakamani kuanzia leo ambapo atakutana ana kwa ana na waendesha mashitaka wa Uswisi wakati akiyajibu maswali katika kesi mbili kati ya msururu wa nyingine ambazo zingali zimeligubika kandanda la dunia na viongozi wake wa zamani na wa sasa.
Platini anahojiwa na leo na kesho mjini Bern, kuhusu kesi ya rushwa ambayo iliiuwa kabisa ndoto yake ya kuchukua usukani wa shirikisho la kandanda duniani – FIFA baada ya kuangushwa kwa Sepp Blatter. Kisha Jumatano, anatarajiwa mjini Sarnen, lakini mara hii akiwa kama shahidi katika uchunguzi kuhusiana na vitendo vya mtu ambaye badala yake alichukua usukani wa FIFA, Gianni Infantino. Wakati Blatter aliangushwa kama mkuu wa FIFA 2015, akamchukua na yule ambaye angekuwa mrithi wake na mkuu wa UEFA; Platini. FIFA ikawapiga wote marufuku kutoka kandanda. Kesi ya Platini inahusiana na malipo ya faranga milioni 2 za Uswisi kutoka FIFA yaliyoidhinishwa na Blatter mwaka wa 2011.
AFP, DPA, AP, Reuters