1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Pentagon yamnasa mtu anayeshukiwa kuvujisha nyaraka za siri

Sylvia Mwehozi
14 Aprili 2023

Maafisa wa shirika la upelelezi wa ndani la Marekani FBI wamemkamata kijana wa miaka 21 anayeshukiwa kuhusika na uvujishaji mkubwa wa nyaraka za siri ikiwemo vita vya Ukraine na Marekani kuwachunguza washirika wake.

https://p.dw.com/p/4Q1ww
USA Dighton | Verhaftung im Zusammenhang mit den US-Leaks
Picha: WCVB-TV/AP/picture alliance

Akizungumza na vyombo vya habari, Mwanasheria Mkuu wa Marekani Merrick Garland amemtaja mshukiwa huyo kuwa ni Jack Teixeira, mfanyakazi katika jeshi la anga la walinzi wa taifa na kiongozi wa kundi la mtandaoni ambako hati hizo zilivujishwa kwa mara ya kwanza.

Kukamatwa kwake kulikotangazwa moja kwa moja na Televisheni, kunafuatia kukamilika kwa uchunguzi wa wiki nzima uliochochewa na ripoti za vyombo vya habari vya Marekani katika mojawapo ya uvujaji mbaya zaidi wa taarifa za siri tangu sakata la Edward Snowden mwaka 2013.

Soma pia: Urusi yatilia mashaka nyaraka za siri za Marekani zilizovuja

Marekani, Washington | Kuvuja kwa nyaraka za siri | Mwanasheria Mkuu wa Marekani Merrick Garland
Mwanasheria Mkuu wa Marekani Merrick GarlandPicha: Evan Vucci/AP Photo/picture alliance

Ofisi ya jeshi la anga la walinzi wa taifa la Marekani imesema kuwa Teixeira alijiunga mwaka 2019 na alikuwa ni mtaalamu wa Tehama ambaye alikuwa amefikia kiwango cha wafanyakazi wa daraja la kwanza. Wizara ya ulinzi ya Marekani Pentagon ilikuwa imesema kuwa kuvuja kwa taarifa hizo kunatoa "hatari kubwa" kwa usalama wa taifa wa nchi hiyo.

Kukamatwa kwa Teixeira kumetokea siku moja baada ya gazeti la The Washington Post kuripoti kuwa mamia ya kurasa za nyaraka zilikuwa zimewekwa kwenye mtandao wa kijamii wa Discord na mtu ambaye alikuwa akifanya kazi katika kambi ya kijeshi ya Marekani.

Gazeti jingine la The New York Times, liliripoti kwamba "nyendo za ushahidi wa kidijitali" zinapendekeza Teixeira kama kiongozi wa kundi la kwenye mtandao wa Discord, linaloitwa Thug Shaker Central, ambako hati hizo zilivujishwa.

Tukio hilo la aibu la kuvuja kwa taarifa za kiusalama, zinazohusisha nyaraka nyeti, limeanika wasiwasi wa Marekani juu ya uwezekano wa uvamizi wa vikosi vya Kyiv dhidi ya wanajeshi wa Urusi, wasiwasi juu ya ulinzi wa anga wa Ukraine na uwezekano kwamba Marekani inawachunguza washirika wake ikiwemo Israeli na Korea Kusini.

Marekani-kuvuja kwa nyaraka-kijana wa miaka 21 akamatwa
Polisi wakiwa wamezuia mtaa mjini MassachusettsPicha: Michelle R. Smith/AP/dpa/picture alliance

Nyaraka zingine ni pamoja na tathmini kwamba Ufaransa inawezekana ikashindwa kufikia malengo ya kiusalama katika kanda ya Afrika magharibi na kati na taarifa kuhusu mpango wa maafisa wa Brazil kutembelea Moscow mwezi Aprili kujadili mpango wa upatanishi wa Ukraine.

Rais Joe Biden alizungumzia tukio hilo mapema siku ya Alhamisi wakati wa ziara yake nchini Ireland, akisema "ana wasiwasi" lakini mamlaka za shirikisho "zinakaribia" kubaini chanzo cha uvujaji huo. Mtu anayeshukiwa kuwa mvujishaji ambaye alijipachika jina la utani la "OG" alikuwa akichapisha nyaraka mara kwa mara katika kundi la mtandaoni. Kundi hilo lenye wanachama wapatao 24 wakiwemo baadhi kutoka Urusi na Ukraine waliunganika kutokana na "kupenda kwao bunduki, zana za kijeshi na Mungu", limeripoti gazeti la The Washington Post.

Nyaraka hizo ziliwekwa kwenye tovuti ya mtandao wa Discord tangu mwezi Machi ama kabla ya hapo lakini hazikusambaa hadi wiki iliyopita.