Patashika ya siku ya mwisho Bundesliga
15 Mei 2017Nafasi mbili za kwanza na mbili za mwisho katika ligi kuu ya kandanda hapa Ujerumani - Bundesliga sasa zimejulikana lakini bado kuna mambo mengine mengi ambayo yatakamilika kaika siku ya mwisho ya msimu ambayo ni Jumamosi ijayo.
Baada ya siku ambayo mechi tisa zilizaa mabao 37 – ikiwa ni idadi kubwa kabisa kuwahi kushuhudiwa katika siku moja ya mechi msimu huu, Ingolstadt ilijiunga na Darmstadt katika kushushwa ngazi wakati RB Leipzig walijihakikishia nafasi ya pili katika msimu wao wa kwanza kabisa kwenye ligi kuu. Leipzig walikuwa kifua mbele 3-1 na 4-2 dhidi ya Bayern, lakini Bayern – ambao tayari walitwaa Kombe lao la tano la Bundesliga mfululizo – wakafunga la tatu katika dakika za mwisho mwisho na mengine mawili katika muda wa nyogeza.
SV Hamburg ilikuwa imelimwa moja bila na Schalke na ilikuwa inakodolea macho kichapo ambacho kingeiweka pabaya sana. Lakini ikaweza kutoka sare ya 1-1 katika dakika ya mwisho. Sare hiyo iliitimua Ingostadt iliyotoka sare ya 1-1 na Freiburg katika Bundesliga.
Wolfsburg walikabwa kwa sare ya 1-1 nyumbani na Borussia Moenchengladbach na watahitaji pointi moja dhidi ya Hamburg wiki ijayo ili kubaki katika Bundesliga (ijapokuwa kichapo kinaweza kuwatosha tu kwa kutegemea matokeo ya mchauno wa Augsburg na Hoffenheim)
Augsburg wana pointi moja na Wolfsburg lakini wanawazidi na bao moja. Augsburg walitoka sare ya 1-1 dhidi ya Borussia Dortmund.
Mainz pia wana pointi sawa lakini wanaokana kuwa salama kabisa kwa sababu ya faida kubwa ya mabao.
Pointi waliyopata Dortmund inawaacha katika nafasi ya tatu, pointi moja na Hoffenheim ambao waliwazaba Erder Bremen 5-3 katika kinyang'anyiro cha kupata tikiti ya moja kwa moja ya Champions League.
Kichapo cha Bremen hakijamaliza kabisa matumaini yao ya kucheza katika Europa League lakini wanaopigiwa upatu kupata nafasi hizo mbili za kufuzu, nambari tano Hertha Berlin, ambao walishinda 2-0 dhidi ya Darmstadt, nambari sita Freiburg na nambari saba Cologne, waliotoka sare ya 2-2 na Bayer Leverkusen.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Iddi Ssessanga