PARIS. Mwenyekiti wa kwanza wa benki kuu ya Ulaya afariki dunia
1 Agosti 2005Mwenyekiti wa kwanza wa benki kuu ya ulaya bwana Wim Duisenberg amefariki.
Habari zimesema kuwa marehemu Duisenberg alipatikana amefariki katika kidimbwi cha kuogelea nyumbani kwake kusini mwa Ufaransa.
Polisi nchini Ufaransa wamesema watatoa taarifa baada ripoti ya uchunguzi wa chanzo cha kifo chake kutolewa.
Waziri wa fedha wa Ujerumani Hans Eichel amemtaja marehemu Duisenberg aliyefariki akiwa na umri wa miaka 70 kama mstahiki aliye toa mchango mkubwa wa kuanzishwa kwa sarafu ya Euro na uthabiti wa uchumi wa ulaya.
Bwana Wim Duisenberg alikuwa mwenyekiti wa benki kuu ya ulaya kuanzia mwaka 1998 hadi mwaka 2003 alipojiuzulu wadhfa wake.
Alizaliwa tarehe 9 julai mwaka 1935 mjini Heerenveen kaskazini mwa Netherlands aliwahi pia kuwa waziri wa fedha mnamo mwaka 1973 na 1977.
Waziri wa fedha wa Ufaransa Thierry Breton amesema marehemu alikuwa mfanyakazi bora wa Ulaya nzima.
Waziri mkuu wa Udachi Jan Peter Balkenende ametoa rambirambi zake kwa mjane na watoto wa bwana Duisenberg.