Papa Francis awasili Indonesia
3 Septemba 2024Ziara hii ni ya 45 ya kiongozi huyo wa kanisa katoliki nje ya nchi,ambayo inalenga kuhimiza amani na mshikamano kati ya dini mbalimbali.
Kwa kuzingatia umri na hali ya afya ya Papa Francis, ambaye sasa mara nyingi hutumia kiti cha magurudumu, muda wa mapumziko baada ya safari zake za kigeni umekuwa mrefu zaidi.
Papa aliwapungia mkono watu wengi waliojitokeza kumlaki kando ya barabra wakati wa msafara wake.
Akibubujikwa na machozi Maria Celine, alielezea furaha yake baada ya kumuona kiongozi huyo wa kidini.
"Ninajivunia na kuguswa sana kwa sababu tuko katika nchi ya Kiislamu na bado tunatembelewa na papa, kiongozi mkuu wa Kikatoliki."
Uwiano wa kidini
Katika ziara hiyo ya siku 12 Papa Francis atazitembelea pia Papua New Guinea,Timor ya Mashariki na Singapore.
Papa atapumzika mjini Jakarta, kisha kukutana na Rais Joko Widodo kesho Jumatano katika sehemu kuu ya kwanza ya ziara yake katika nchi hiyo yenye Waislamu wengi zaidi duniani.
Indonesia inahesabika kuwa nchi yenye idadi kubwa ya waislamu duniani, wanaofikia milioni 240 wakati Timor mashariki ndiyo yenye idadi kubwa ya wakristo katika nchi ambazo Papa Francis atazitembelea.
Mkutano na viongozi wa kidini
Siku ya Alhamisi, Papa Francis atakutana na wawakilishi wa dini au madhehebu sita yanayotambulika rasmi nchini Indonesia katika Msikiti mkubwa zaidi Kusini-mashariki mwa Asia wa Istiqlal, ishara ya uwiano wa pamoja kidini.
Kulingana na maaskofu wa Indonesia, katika Msikiti wa Istiqlal, Papa Francis anatarajiwa kutia saini tamko la pamoja na imamu mkuu, ambalo litazingatia kupinga udhalilishaji, haswa kutokana na kuenea kwa ghasia na migogoro, pamoja na uharibifu wa mazingira.
Kisha ataongoza misa na kutoa mahubiri katika uwanja wa taifa wa kandanda wenye uwezo wa kuchukua watu 80,000.
Lakini licha ya Indonesia kutambuwa rasmi imani tofauti, kuna wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa ubaguzi, ikiwa ni pamoja na dhidi ya Wakristo, huku Wakatoliki wa eneo hilo wakitumai papa atazungumza changamoto hiyo.
Ziara hii ya Papa Francis nchini Indonesia ni ya tatu kuwahi kufanywa na papa na ya kwanza tangu John Paul II mwaka 1989. Hapo awali ilipangwa kwa 2020 lakini iliahirishwa kutokana na janga la UVIKO.