1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Francis awaonya wanaokataa chanjo

10 Januari 2021

Maaambukizi ya virusi vya Corona yakiongezeka barani Ulaya kiongozi mkuu wa kanisa katoliki duniani Papa Francis amewaonya wanaokataa kupata chanjo dhidi ya virusi hivyo kwamba wanayaweka rehani maisha yao na ya wengine

https://p.dw.com/p/3nkWn
Vatikan Petersdom Papst Franziskus Segen "Urbi et orbi"
Picha: Vatican Media/AP Photo/picture alliance

Kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Francis ameiita hatua ya watu kukwepa kupata chanjo ya Covid-19 ni mauaji ya kujitakia akisema wale wanaokataa chanjo hiyo wanacheza na afya zao na pia maisha ya watu wengine.

Kiongozi huyo mkuu wa kidini kwa upande mwingine amethibitisha kwamba binafsi atapata chanjo hiyo mwanzoni mwa wiki ijayo huku akiwaita watu wanaopinga chanjo hiyo kuwa wenye kupingana na kifo. Papa Francis akizungumza na shirika la habari la Italia amewatolea mwito watu kujitokeza kupata chanjo hiyo akisema kwamba anaamini kimaadili kila mmoja anapaswa kupata chanjo.

Amesisitiza kwamba ni uamuzi wa kimaadili wa mtu binafsi kwasababu ni sawa na kucheza mchezo wa kubahatisha na afya yako,maisha yako lakini pia unayaweka rehani maisha ya watu wengine.

Großbritannien Oxford | Coronavirus | AstraZeneca Impfstoff
Picha: Steve Parsons/empics/picture alliance

Kiongozi huyo wa kiimani wa kanisa katoliki duniani mwenye umri wa miaka 84 binafsi hana sehemu moja ya mapafu kitu ambacho kinamfanya kuwa miongoni mwa watu walioko kwenye hatari kubwa wakiambukizwa virusi hivyo.  Makao makuu ya kanisa hilo,Vatican awali yalitangaza kwamba ni hatua inayokubalika kimaadili kwa waumini wa kanisa hilo kupata chanjo dhidi ya virusi hivyo ambayo utafiti wake umehusisha matumizi ya seli zilizochukuliwa kwenye tishu zilinazotokana na mimba zilizoharibiwa.

Harakati za kutowa chanjo ndani ya Vatican zinaanza wiki ijayo wakati ikiripotiwa kwamba kuna alau visa 27 vya maambukizi vilivyothibitishwa kwenye eneo hilo. Ama barani Ulaya huko Ubelgiji idadi ya waliokufa kutokana na virusi hivyo imefikia zaidi ya watu 20,000 kufikia Jumapili.

Großbritannien Oxford | Coronavirus | AstraZeneca Impfstoff
Picha: Steve Parsons/empics/picture alliance

Ufaransa jumamosi iliweka sheria kali zaidi katika mikoa mbali mbali,hatua ambazo zinajumuisha kutotea nje usiku. Nchini Ujerumani jumla ya vifo kutokana na ugonjwa huo imepindukia 40,000 huku kansela Angela Merkel akionya kwamba wiki zinazokuja hali itakuwa ngumu zaidi. Katika kipindi cha saa 24 zilizopita vifo 465 vimeripotiwa Ujerumani.

Na nchini Japan  watu wanne waliowasili kutoka Brazil wamegundulika kuwa na maambukizi ya virusi aina mpya vya Corona ambavyo ni tofauti kabisa na vile vilivyogunduliwa Uingereza.

Mwandishi Saumu Mwasimba

Mhariri:Saumu Njama

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW