Papa Francis ahimiza amani katika hotuba yake ya Pasaka
17 Aprili 2022Papa Francis amewataka viongozi kusikia vilio vya watu wanaotaka amani nchini Ukraine. Amesema amesikitishwa kuwa Pasaka ya mwaka huu ni Pasaka iliyogubikwa na vita.
Papa Francis ameilaumu tabia ya kutunishiana misuli huku watu wakiwa wanateseka nchini Ukraine lakini bila ya kumlaumu waziwazi Rais wa Urusi Vladimir Putin kwa uamuzi wake wa kuanzisha uvamizi na mashambulio dhidi ya Ukraine mnamo Februari 24.
Akizungumza na takriban watu 50,000 waliohudhuria ibada hiyo ya Jumapili ya Pasaka katika kanisa la mtakatifu Peter, katika misa anayoiongoza mara mbili kwa mwaka ya "Urbi et Orbi" kwa ajili ya jiji la Vatican na ulimwengu kwa jumla, Papa Francis amesema Ukraine inakabiliwa na mtihani mkubwa sana wa kukumbwa na ghasia na uharibifu kutokana na vita vya kikatili visivyostahili kuwepo.
Papa Francis mwenye umri wa miaka 85 kwenye sehemu kubwa ya hotuba yake, amezungumza juu ya migogoro ya dunia, pamoja na mgogoro wa sasa wa nchini Ukraine.
Papa Francis ameeleza kwamba mzozo huu wa barani Ulaya uwafanye watu wawe na wasiwasi zaidi kuhusu nchi zingine zinazokabiliwa na migogoro, mateso na huzuni, hali ambazo zinaathiri maeneo mengi ulimwenguni. Miongoni mwa migogoro aliyotaja ni ile ya Mashariki ya Kati na amehimiza amani na upatanisho kwa watu wa Lebanon, Syria na Iraq. Pia ameyazugnumzia mataifa ya Libya na Yemen ambayo yanakabiliwa na migogoro inayoonekana kusahaulika na wote.
Vile vile Papa Francis katika siku ya Jumapili ya Pasaka ametoa wito wa kufunguliwa njia kwa watu kuyafikia maeneo matakatifu katika mji wa Jerusalem wakati ambapo ghasia zinaendelea kati ya Waisraeli na Wapalestina katika Jiji hilo Takatifu.
Amesema anaomba amani iwepo katika Mashariki ya Kati, iliyogubikwa na mizozo na migawanyiko kwa miaka mingi. Hususan katika siku hii tukufu, Papa Francis amemtaka kila mtu aombe amani katika mji wa Jerusalem kwa wote Wakristo, Wayahudi na Waislamu wanaokaa katika jiji takatifu, pamoja na mahujaji na wakati huo huo amesisitiza umuhimu kwa jamii kukaa katika udugu na kufurahia nafasi ya kufika bila masharti yoyote mahala patakatifu kwa kuheshimianana kuzingatia haki za kila mmoja.
Vyanzo:AP/AFP/DPA