Papa Francis aendelea na ziara huko Papa New Guinea
7 Septemba 2024Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis ametoa wito kwa viongozi wa Papua New Guinea kwamba utajiri mkubwa wa rasilimali za nchi hiyo lazima unufaishe jamii nzima.
Francis ametoa kauli hiyo wakati alipokutana na wanasiasa, wanadiplomasia na viongozi wa asasi za kiraia nchini humo akisema mali zote zimetolewa na Mungu kwa ajili ya watu wote. Kiongozi huyo wa kidini alikutana na viongozi hao katika siku ya kwanza ya ziara yake kwenye taifa hilo la Pasifiki Kusini.
Matamshi yake huenda yakaongeza shinikizo kwa viongozi wa Papua New Guinea na kuwatia moyo wananchi wanaoamini maliasili za nchi hiyo zinafujwa au kuibiwa. Papua New Guinea ina utajiri mkubwa wa madini ya dhahabu, shaba, nikeli, gesi asilia na mbao ambavyo vimeyavutia makampuni kadhaa ya kimataifa kwa uwekezaji.