Papa Francis aruhusiwa kutoka hospitalini
1 Aprili 2023Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis, ameruhusiwa kutoka hospitalini leo, baada ya kulazwa kwa siku tatu kwa ajili ya matibabu ya ugonjwa wa kifua na sasa anatarajiwa kuanza maandalizi ya wiki muhimu zaidi katika kalenda ya Kikristo. Papa huyo mwenye umri wa miaka 86 alilazwa siku ya Jumatano katika hospitali ya Gemelli mjini Rome baada ya kukumbwa na matatizo ya kupumua. Hapo jana, kiongozi huyo alitembelea wadi ya watoto wanaougua saratani hospitalini hapo na kutoa zawadi za Pasaka pamoja na kutoa ubatizo. Papa Francis anatarajiwa kuongoza misa ya Jumapili ya Matawi katika uwanja wa St. Peter. Misa hiyo inaashiria kuanza kwa wiki takatifu, ambayo kilele chake ni Sikukuu ya Pasaka. Papa Francis alitimiza miaka 10 kama kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani mapema mwezi uliopita.