1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Francis akosoa kuibuka tena kwa vita

26 Septemba 2024

Kiongozi wa kanisa Katoliki duniani Papa Francis, leo ameanza ziara ya siku nne nchini Luxembourg na Ubelgiji akitoa wito wa diplomasia ya kimataifa na mashauriano huku kukiwa na wimbi la mizozo kote ulimwenguni.

https://p.dw.com/p/4l7Yz
Papa Francis
Kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Francis Picha: Omar Havana/AP Photo/picture alliance

Papa Francis anapanga kuutumia muda wake katika nchi hizo mbili ambazo zina taasisi muhimu za juu za Ulaya kujadili jukumu la bara hilo ulimwenguni.

Papa atoa wito wa kuwepo amani duniani

Baada ya mkutano na maafisa katika ikulu ya Grand Ducal mjini Luxembourg, baba mtakatifu Francis amekosoa "kuibuka tena, hata katika bara la Ulaya, kwa mipasuko na udhalimu unaosababisha uhasama wa wazi, ambao nao husababisha uharibifu na vifo.

Papa amesema Luxembourg inaweza kumuonyesha kila mtu manufaa ya amani kinyume na vitisho na maovu ya vita, akidokeza kuhusu utajiri wa nchi hiyo na jukumu lake kama ngome ya demokrasia na makao ya taasisi nyingi za Ulaya.