Papa Francis akemea kashfa ya unyanyasaji wa kingono Ureno
3 Agosti 2023Papa Francis alijitosa katika mgogoro unaolitikisa kanisa la Ureno kwenye siku ya kwanza ya ziara yake ya siku tano mjini Lisbon ambako atahudhuria tamasha la Kanisa Katoliki la Siku ya Vijana Duniani
Ziara yake inajiri katika wakati mgumu kwa kanisa la Ureno, ambapo jopo la wataalamu lililoteuliwa na maaskofu wa Ureno liliripoti Februari kuwa makasisi na viongozi wengine wa kanisa huenda waliwadhalilisha karibu wavulana na wasichana 4,815 kati ya mwaka wa 1960 na 2022. Uchunguzi huo, ulihitimisha kuwa uongozi wa Kanisa ulijaribu kuficha unyanyasaji huo.
Soma pia: Papa aitaka Ulaya kufanya zaidi kutatua matatizo ya dunia
Makao makuu ya Vatican yamesema Francis alikutana na waathiriwa 13 wa unyanyasaji wa kingono uliofanywa na mapadri katika kikao kilichodumu kwa zaidi ya saa moja kwenye ubalozi wa Vatican. Waliandamana na wawakilishi wa taasisi za kanisa la Ureno zinazoshughulika na mipango ya ulinzi wa Watoto.
Mkutano huo ulijiri baada ya Papa Francis kuwakemea viongozi wa Kanisa Katoliki la Ureno kwa kashfa ya unyanyasaji wa kingono unaowahusisha mapadri. Alisema vitendo vya mapadri hao vimechangia kuwafukuza waumini na akawaamuru viongozi wa kanisa Katoliki kubadili mienendo yao na kuwajali zaidi wahanga wa maovu hayo. Akizungumza katika Kihispania, Papa Francis alikiri kuwa mapadri wengi na watawa katika nchi ambazo wakati mmoja zilikuwa na parokia zilizokuwa zinaendeshwa vyema wanahisi uchovu kuhusu miito yao kwa sababu waumini wanaendelea kujitenga na Imani yao.
"Na uchovu huo mara nyingi huchangiwa na kukatishwa tamaa au hasira ambayo wengine wanayo kuhusiana na Kanisa. Katika baadhi ya matukio, kutokana na sifa yetu mbaya na kashfa ambazo zimeharibu picha ya kanisa, na kashfa hizo zinahitaji utakaso wa unyenyekevu na wa mara kwa mara, kuanzia kilio cha maumivu ya waathiriwa ambao wanapaswa kukaribishwa na kusikilizwa kila wakati.
Awali, Francis mwenye umri wa miaka 86, aliikosoa Ulaya kwa kutofanya juhudi za kutosha ili kutatua matatizo ya ulimwengu.
Akizungumza na wawakilishi wa serikali ya Ureno na mashirika ya kiraia, papa alishutumu kutokuwepo kwa mpango dhabiti wa amani na kusema fedha zaidi zinawekezwa katika silaha kuliko katika mustakabali wa watoto. "Kwa maana dunia inaihitaji Ulaya, Ulaya ya kweli. Inahitaji jukumu la Ulaya kama daraja na mtunza amani katika upande wake wa mashariki, katika bahari ya Mediterania, Afrika na Mashariki ya Kati. Kwa njia hii, Ulaya itaweza kutoa mchango wake mahususi katika nyanja ya kimataifa, na uhalisi wake mahususi."
Francis yuko Lisbon kushiriki Siku ya Vijana Ulimwenguni, tamasha la kikatoliki la siku tano lililoanzishwa na Mtume Paul John II katika miaka ya 1980 ili kutia nguvu kizazi kijacho cha Wakatoliki katika imani yao. Ni tamasha la kwanza kufanyika tangu kuzuka janga la UVIKO-19. Kilele cha ziara yake ni pamoja na ibada za maombi Jumamosi na Jumapili.
AP, AFP, DPA, Reuters