1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Francis akamilisha ziara ya siku sita barani Afrika.

6 Februari 2023

Kiongozi wa Kanisa Katoliki, Papa Francis amerejea Vatican siku ya Jumapili baada ya kukamilisha ziara yake ya siku sita katika nchi za Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Sudan Kusini.

https://p.dw.com/p/4N7Zu
Südsudan Juba Besuch von Papst Franziskus
Picha: Ben Curtis/AP/picture alliance

Akiwa Sudan Kusini, nchi inayokumbwa na vita, Papa Francis aliwataka raia na wanasiasa kuiombea nchi yao amani. Pia alionyesha huruma yake kwa mamilioni ya wakimbizi wa Sudan Kusini walioko nje na waliogeuka kuwa wakimbizi wa ndani. Sudan Kusini ilikuwa kituo cha pili katika ziara ya Papa Francis barani Afrika baada ya kuitembelea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis.
Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis.Picha: Vatican Media/abaca/picture alliance

Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis amemaliza ziara yake nchini Sudan Kusini pia kwa kuwatolea mwito watu wa nchi hiyo kujiepusha na matendo ya chuki. Amewataka wajitahidi kufikia amani na kuendeleza ustawi wa nchi yao ambayo kwa miaka mingi imekumbwa na migogoro ya kikabila iliyosababisha umwagikaji damu.

Soma:Papa Francis awasili nchini Sudan Kusini

Kabla ya kupanda ndege kurejea nyumbani, Papa Francis aliongoza Misa kwenye eneo la wazi ambako umejengwa mnara kwenye kaburi la shujaa wa ukombozi wa Sudan Kusini, John Garang, aliyefariki mwaka 2005.

 Shujaa wa ukombozi wa Sudan Kusi marehemu John Garang.
Shujaa wa ukombozi wa Sudan Kusi marehemu John Garang.Picha: AP

Makao makuu ya kanisa katoliki mjini Vatican yamesema watu wapatao 100,000 walihudhuria Misa hiyo.

Papa Francis mwenye umri wa miaka 86 alisisistiza kwenye mahubiri yake mada zilizotawala safari yake kwa taifa jipya zaidi duniani la Sudan kusini, ambazo ni upatanisho na kusameheana makosa yaliyopita. Aliwaomba waumini waepukane vurugu zinazosababishwa na ghadhabu potofu.  Papa pia aliwashukuru watu wa Sudan Kusini kwa ukarimu waliyomwonyesha.

Soma:Papa: Makanisa yapaze sauti dhidi ya dhuluma Sudan Kusini

Kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Francis kwa muda mrefu ameguswa na hali ya nchini Sudan Kusini. Alidhihirisha hilo kwenye hatua moja ya ishara ya ajabu katika upapa wake pale alipopiga magoti na kubusu miguu ya viongozi wa nchi hiyo Salva Kiir na Riek Machar waliokuwa mahasimu wakati wa mkutano wa mjini Vatican mnamo mwaka 2019.

Papa Francis aliandamana na viongozi wawili wa kanisa la Kiprotestanti kutoka Uingereza, Askofu Mkuu wa Canterbury Justin Welby ambaye ni kiongozi wa kimataifa wa Usharika wa Kanisa la Anglikana, na lain Greenshields, Msimamizi wa Baraza Kuu la Kanisa la Scotland.

Hii ilikuwa ni ziara ya kwanza ya Papa Francis katika nchi ya Sudan Kusini tangu ilipopata uhuru wake kutoka Sudan mnamo mwaka 2011.

Kushoto. Papa Francis. Kulia: Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir Mayardit.
Kushoto. Papa Francis. Kulia: Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir Mayardit.Picha: Vatican Media/REUTERS

Lakini licha ya shamrashamra za kupata uhuru huo, Sudan Kusini ilitumbukia vitani kati ya makundi ya ndani miaka miwili baadaye katika mzozo ambao ulisababisha vifo vya watu wapatao 400,000 na wengine karibu milioni nne walilazimika kukimbia makazi yao.

Mkataba wa amani ulitiwa saini mnamo mwaka wa 2018 kati ya Rais Salva Kiir na naibu wake Riek Machar lakini mpaka sasa mengi miongoni mwa masharti yaliyowekwa bado hayajatimizwa na ghasia zinaendelea kuikumba nchi hiyo.

Vyanzo:DPA/RTRE/AFP/AP