Papa Francis aibua mjadala Marekani
19 Februari 2016"Mtu yeyote, hata kama ni nani ambaye anataka kujenga ukuta badala ya daraja huyo siyo mkiristo" Papa Francis aliwaambia hayo waandishi wa habari mara baada ya kumaliza ziara yake nchini Mexico.
Kiongozi huyo mkuu wa kikatoliki duniani alitoa kauli hiyo pale alipokuwa akijibu swali la mwandishi wa habari aliyetaka kupata maoni yake kuhusiana na kile kinachoweza kuwa msimamo wa chama cha Republican unaoonekana kupinga suala la kuwapokea wakimbizi, ambapo alisisitiza kwa kusema kuwa mtu yeyote anayetoa kauli ya aina hiyo hawezi kuwa mkiristo.
" Tunataka kujiridhisha iwapo kweli alitoa kauli hiyo, hivyo nasubiri kuthibitisha" aliongeza Papa Francis.
Licha ya ufafanuzi huo, bado kauli hiyo ya Papa Francis imeshutumiwa vikali na mfanya biashara huyo tajiri wa kimarekani anayetafuta nafasi ya kuteuliwa kupitia chama cha Republican kuwa mgombea wa nafasi ya urais wa Marekani katika uchaguzi utakaofanyika baadaye mwaka huu.
Trump aonyesha kukerwa na kauli ya Papa Francis
" Kwa kiongozi wa dini kutoa matamshi ya aina hiyo ni kitendo cha fedheha " alisema Donald Trump katika kauli yake aliyoitoa wakati wa mkutano wa kampeni katika jimbo la South Carolina ambako chama hicho kitakuwa na chaguzi za awali mwishoni mwa wiki hii.
Alisisitiza kuwa anajivunia kuwa mkiristo na kama mkiristo hatakuwa tayari kuona ukiristo unashambuliwa au kudhooofishwa.
Donald Trump amejizolea umaarufu katika siku za hivi karibuni kutokana na kauli yake ya kudai kuwa Mexico inaingiza watu ambao ni wahalifu nchini Marekani na juma lililopita alimshutumu Papa Francis kwa kutembelea eneo la mpaka kati ya Marekani na Mexico.
Papa Francis alitoa matamshi hayo mara baada ya kukamilisha ziara yake ya siku tano nchini Mexico ambapo aliendesha misa iliyoshirikisha kiasi ya watu 300,000 karibu na mpaka na Marekani, na kusema ni janga la kibinadamu ulimwengu unaposhuhudia wahamiaji wanaokimbia mapigano kutoka maeneo mbalimbali duniani.
Mfanya biashara huyo maarufu tayari ameahidi katika mikutano yake ya kampeni ya kuwa atajenga ukuta katika eneo la mpaka la upande wa kusini nchini humo ili kuwazuia wahamiaji wanaoingia nchini Marekani kinyume cha sheria , kauli ambayo imeibua mjadala mkali katika mikutano ya kampeni ambayo imekuwa ikiendelea nchini humo.
Trump aliongeza kuwa iwapo makao makuu ya kanisa Katoliki duniani yakishambuliwa na dola la Kiislamu kitu ambacho kila mmoja ana jua ndio ushindi mkubwa unaotafutwa na IS basi baba mtakatifu angetamani sana na kuomba kuwa Donald Trump angekuwa Rais.
Aidha Trump alisema viongozi wa Mexico wamemueleza Papa Francis upande mmoja tu wa suala hilo bila kumfahamisha juu ya madhara yanayosababishwa na sera hizi zinazohusiana na wahamiaji.
Wakati huohuo akijibu swali iwapo ni sahihi kutumia mbinu za kuzuia kupata uja uzito au kutoa ujauzito ili kuzuia kuenea kwa maambukizi ya kirusi cha Zika , baba mtakatifu alijibu na kusema kuwa kitendo cha kutoa mimba ni uhalifu kwani unaondoa uhai wa kiumbe kimoja ili kuokoa maisha ya kiumbe kingine na kusisitiza kuwa hiyo ni dhambi kubwa sana.
Hata hivyo kwa upande mwingine alisema kuzuia kupata uja uzito sio dhambi kauli ambayo imewahi pia kutolewa na Papa Paul wa VI kwa watawa ambao wanakabiliwa na kitisho cha kupata uja uzito kuwa wanapaswa kutumia njia za kuzuia kupata uja uzito.
Hata hivyo baba mtakatifu aliwataka madakitari kufanya kila jitihada kuhakikisha kuwa wanapata chanjo ya kukabiliana na maradhi yanayosababishwa na kirusi hicho cha Zika.
Mwandishi: Isaac Gamba/ AFPE/ DPAE
Mhariri: Iddi Ssessanga