Papa Francis afanya maombi nchini Canada
27 Julai 2022Ibada hiyo ya maombi katika ziwa la Mtakatifu Anne huko Alberta iliyowakusanya zaidi ya waumini 10 000 huku wengine wakisafiri kwa umbali mrefu, ilikuwa moja ya matukio muhimu ya kiroho ya ziara ya siku sita ya Papa Francis nchini Canada, ili kulitakasa Kanisa Katoliki na matendo yake katika shule za bweni ambazo ziliwashinikiza kwa nguvu watoto wa jamii ya wenyeji wa asili kujiunga na jamii ya Kikristo. Papa Francis aliomba kwa ajili ya uponyaji wa jamii hiyo:
"Bwana, kama vile watu wa pwani ya bahari ya Galilaya hawakuogopa kukulilia na mahitaji yao, ndivyo tunakuja kwako jioni hii na maumivu yote tunayobeba ndani mwetu. Tunakuletea wasiwasi wetu na majeraha ya unyanyasaji wa kaka na dada zetu wa jamii ya wenyeji wa asili. Katika sehemu hii iliyobarikiwa ambapo maelewano na amani vinatawala, tunawasilisha kwako athari mbaya za ukoloni, uchungu wa familia nyingi. Bwana, tusaidie kuponya majeraha yetu. Tunajua kwamba hili linahitaji juhudi kubwa, uangalifu na matendo madhubuti, lakini pia tunajua Bwana, kwamba hatuwezi kufanya hili peke yetu."
Soma zaidi:Papa Francis aomba radhi kwa makosa ya Kanisa nchini Canada
Msamaha wa Papa Francis
Siku ya Jumatatu Papa Francis aliomba msamaha kwa "aina mbaya" familia hizo zilisambaratika huku siku iliyofuata akijikita na maombi ya kuwasaidia wenyeji hao kufikia uponyaji wa kile alichokiita "majeraha ya ukatili."
Sherehe hizo ziliambatana na Sikukuu ya Mtakatifu Anne, bibi wa Yesu Kristo na kielelezo kikuu cha ibada maalum kwa jamii ya wenyenji wa asili na Wakatoliki, ambao kila mwaka hufanya hija katika ziwa la Mtakatifu Anne.
Papa Francis alisisitiza umuhimu wa mabibi katika familia za wenyeji hao wa asili, na akakumbusha jukumu muhimu la bibi yake Rosa aliyemrithisha mikoba ya kiimani alipokuwa bado kijana huko Buenos Aires nchini Argentina.
Soma zaidi: Papa Francis kuwaomba radhi wenyeji wa asili wa Canada
Historia "mbaya" ya kikatili
Zaidi ya watoto 150,000 wa jamii ya wenyeji wa asili nchini Canada walilazimishwa kuhudhuria shule za Kikristo zilizofadhiliwa na serikali kutoka karne ya 19 hadi miaka ya 1970, katika jitihada za kuwatenga na ushawishi wa tamaduni zao za asili. Lengo kuu ilikuwa kuwalazimisha kuwa Wakristo na kuwaingiza katika jamii iliyotawala wakati huo na ambayo serikali zilizopita za Canada ziliichukulia kuwa juu ya jamii zingine.
Katika tukio lake la kwanza nchini Canada siku ya Jumatatu, Papa Francis aliomba msamaha katika eneo la shule ya zamani huko Maskwacis kutokana na uovu uliofanywa na Wakristo walio wengi dhidi ya watu wa jamii za asili, na kusisitiza kuwa shule hizo za bweni ilikuwa "kosa kubwa" na iliyoenda kinyume na mafundisho ya dini hiyo.
(APE)