1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Benedict XVI alaumiwa kwa unyanyasaji wa watoto

20 Januari 2022

Ripoti ya utafiti uliofanywa na kampuni moja ya mawakili ya Ujerumani, imefichua kuwa aliyekuwa kiongozi wa kanisa katoliki Benedict XVI alishindwa kushughulikia visa vinne vya unyanyasaji dhidi ya watoto.

https://p.dw.com/p/45qO3
Papst Benedikt XVI
Picha: Sven Simon/imago images

 

Kampuni hiyo ya mawakili ya Westphal Spilker Wastl (WSW), imesema kuwa Papa Benedict alishindwa kuzuia unyanyasaji wa watoto wakati wa uongozi wake kama askofu mkuu wa majimbo ya Munich na Freising kuanzia mwaka wa 1977 hadi 1982. Wakili Martin Pusch aliyewasilisha ripoti hiyo ya WSW, amesema kuwa katika jumla ya visa vinne, waliafikia makubaliano kwamba hatua iliyostahili haikuchukuliwa.

Makasisi wahusishwa katika visa viwili

Visa viwili vinahusisha makasisi ambao walishtakiwa kisheria kwa unyanyasaji wa watoto chini ya askofu huyo wa zamani, ambaye alijulikana kama askofu mkuu Joseph Ratzinger wakati huo. Wawili hao waliruhusiwa kuendelea na kazi yao kanisani kama makasisi.

Kanisa pia halikuchukua hatua rasmi za kinidhamu dhidi ya makasisi hao na inaonekana kwamba waathiriwa wao pia hawakushughulikiwa. Benedict amekanusha mashtaka hayo. Askofu mkuu wa sasa wa Munich Reinhard Marx pia anashtumiwa kwa kushindwa kuingilia kati katika visa hivyo viwili vya unyanyasaji.

Ripoti hiyo ya WSW pia imefichua kutokea kwa takriban visa 497 vya unyanyasaji kati ya mwaka 1945 na 2019. Unyanyasaji mkubwa ulihusisha vijana wadogo. Ripoti hiyo ni kashfa ya hivi karibuni zaidi ya unyanyasaji wa watoto kuathiri Kanisa Katoliki.

Askofu huyo wa zamani akanusha madai

Mapema wiki hii, askofu huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 94 alikanusha kuwa alijua habari kuhusu unyanyasaji wa kijinsia katika shirika la kidini la kikatoliki la Legionaries of Christ lenye makao yake huko Mexico. Mwanzilishi wa shirika hilo la Legionaries of Christ Marcial Macial, aliyefariki dunia mnamo mwaka 2008, ameshtumiwa kwa kuwanyanyasa watoto kadhaa.

Kashfa hiyo ya unyanyasaji wa kijinsia ya shirika la Legionaries of Christ , imechafua mwelekeo na urithi wa Papa John Paul II, aliyeongoza kanisa hilo kuanzia mwaka 1978 hadi kifo chake mwaka 2005. John Paul II alimsifu Maciel na kupigia debe kazi ya Legionaries of Christ katika kipindi chake cha uongozi wa kanisa hilo.