1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiTimor Mashariki

Papa asifu mchakato wa maridhiano Timor Mashariki

10 Septemba 2024

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis ameusifu mchakato wa maridhiano wa baada ya vita uliofanyika nchini Timor Mashariki akiutaja kuwa mfano kwa maeneo mengine yanayokabiliwa na mizozo.

https://p.dw.com/p/4kRVV
Papa Francis akiwa Timor Mashariki
Papa Francis akiwa Timor Mashariki.Picha: Dita Alangkara/AP Photo/picture alliance

Papa Francis ameyasema hayo alipozungumza baada ya kuwasili kwenye taifa hilo dogo la kusini mwa Asia, kituo cha tatu cha ziara yake ndefu ya kuyazuru mataifa manne.

Baba Mtakatifu Francis amesema anatumai maeneo mengine duniani yataiga kile kilichofanywa Timor Mashariki na kwamba Mungu Mwenyezi atafungua milango ya kupatikana amani.

Timor Mashariki ambalo ni koloni la zamani la Ureno lilishuhudia miongo kadhaa ya mapigano ya kupinga kukaliwa kwa mabavu na taifa jirani la Indonesia.

Ukaliaji huo ulioanza katikati ya miaka 1970 ulimalizika mwaka 2002 nchi hiyo ilipotangaza uhuru kutoka Indonesia. Inakadiriwa kati ya wanajeshi na raia 100,000 hadi 180,000 waliuawa vitani au kwa kunyimwa chakula katika kipindi hicho cha karibu miongo mitatu.