1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pande pinzani katika machafuko ya Libya zalaumiana

12 Januari 2020

Kamanda wa LNA amedai wanamgambo wa GNA wamekiuka makubaliano ya kusitisha mapigano kwa kutumia silaha mbalimbali katika maeneo tofauti. Lakini GNA imesema kwenye taarifa kuwa imerekodi mashambulizi ya risasi kutoka LNA.

https://p.dw.com/p/3W4b1
Konflikt in Libyen | Kämpfe
Picha: picture-alliance/dpa/A. Salahuddien

Pande mbili zinazozozana katika machafuko ya Libya zimeelekezeana lawama kwa kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano ambayo yalipendekezwa na Uturuki pamoja na Urusi. Hayo yamejiri baada ya mapigano kushuhudiwa Jumapili katika viunga vya mji mkuu Tripoli.

Rais wa Urusi Vladimir Putin na mwenzake wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan walitoa wito wa kusitisha mapigano kuanzia Jumapili, ikiwa ni miezi tisa tangu vikosi vya mbabe wa kijeshi Khalifa Khaftar vinavyojiita Jeshi la Taifa la Libya (LNA) vyenye makao yao mashariki mwa nchi hiyo kuanza mashambulizi yaliyolenga kuuchukua udhibiti wa mji mkuu Tripoli.

LNA pamoja na serikali ya Makubaliano ya Taifa (GNA) inayotambuliwa kimataifa zilishasema kuwa zimesitisha mashambulizi kwa masharti.

Lakini GNA ilisema kwenye taarifa kuwa imerekodi mashambulizi ya risasi katika maeneo ya Salaheddin na Wadi Rabea, dakika kadhaa baada ya utekelezaji wa makubaliano ya kusitisha mapiano kuanza usiku wa kuamkia Jumapili.

GNA imeongeza kuwa mashambulizi hayo yameshuhudiwa mapema leo katika wilaya za Salaheddin na Ain Zara.

Juhudi za kufikia makubaliano ya kudumu ya kusitisha mapigano Libya huenda zikakumbwa na ugumu kufuatia migawanyiko iliyoko katika miungano ya majeshi ya Libya, huku vikundi tofauti pamoja na wapiganaji wa kigeni wakipelekwa katika pande zote mbili. Kila upande nao unautaja upande mwingine kuwa wanamgambo.

Mapigano ya Libya kati ya serikali inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa pamoja na vikosi vya mbabe wa kivita Khalifa Khaftar yamedumu kwa miezi tisa sasa.
Mapigano ya Libya kati ya vikosi vya serikali inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa pamoja na vikosi vya mbabe wa kivita Khalifa Khaftar yamedumu kwa miezi tisa sasa.Picha: picture-alliance/dpa/A. Salahuddien

Kamanda wa LNA Al-Mabrouk Al-Gazawi amedai kuwa wanamgambo wa GNA wamekiuka makubaliano hayo kwa kutumia silaha mbalimbali katika maeneo tofauti. Al-Gazawi ameongeza kuwa vikosi vyao vinasubiri maelekezo kutoka kwa makao yao makuu.

Nayo serikali ya GNA imesema kwenye taarifa kuwa imerekodi visa vya ukiukaji wa makubaliano hayo ambavyo vimefanywa na wanamgambo wachokozi. Lakini inasisitiza kujitolea kwao kuyaheshimu makubaliano hayo. Imetilia mkazo umuhimu wa wakuu wa pande zote husika pamoja na ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya kuyatekeleza makubaliano hayo kwa ukamilifu

Wizara ya Ulinzi ya Uturuki imesema kuwa imeona pande zote zikijaribu kuyaheshimu makubaliano hayo na kwamba kuna hali ya utulivu isipokuwa tu visa vichache vilivyoshuhudiwa.

Makubaliano ya kusitisha vita yalifikiwa baada ya mapigano kuongezeka hivi karibuni katika viunga vya mji wa Tripoli, pamoja na hatua ya vikosi vya LNA kuelekea katika mji wa Sirte, ambao ni muhimu kimkakati katika pwani ya Libya.

Makubaliano hayo pia yalijiri baada ya Umoja wa Mataifa na mataifa yenye nguvu ya Umoja wa Ulaya kuandaa mkutano wa kilele mjini Berlin uliolenga kumaliza juhudi za kidiplomasia na kuanzisha mchakato uliositishwa wa amani kufuatia mashambulizi ya vikosi vya Haftar.

Upande wa LNA umepata uungwaji mkono kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu, Jordan, Misri na Urusi huku upande wa GNA ukiungwa mkono na Uturuki, ambayo mwezi huu, ilipitisha kwa njia ya kura, hatua ya kuwatuma wanajeshi wake katika taifa hilo la kaskazini mwa Afrika.

Vyanzo: RTRE, DPAE