1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pande hasimu Syria zakutana Geneva kwa mazungumzo

Yusra Buwayhid
31 Oktoba 2019

Pande hasimu katika vita vya wenyewe kwa wenyewe Syria kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka minane na nusu zimekutana Jumatano mjini Geneva, Uswisi, wakijaribu kutunga katiba mpya kumaliza vita.

https://p.dw.com/p/3SFPV
Schweiz Genf | Treffen zum neuen Verfassungsausschuss Syriens | Ahmad Kuzbari, Geir Pedersen und Hadi al-Bahra
Picha: Reuters/D. Balibouse

Wajumbe wapatao 150 walikaa pamoja katika meza ya mazungumzo mjini Geneva, Uswisi. Wajumbe hao 50 ni wawakilishi wa upanade wa serikali, 50 wawakilishi wa upinzani na 50 wengine kutoka asasi za kiraia. Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa Syria,Geir Pederson ameueleza mkutano huo kuwa ni wa kihistoria. Baada ya ufunguzi wa mkutano, wajumbe 45 walianza kufanya kazi ya kuandika rasimu ya katiba kwa lengo la kufikia makubaliano. Mfumo wa upigaji kura wa asilimia 75 utatumika kufanya mabadiliko ikiwa makubaliano hayatowezekana.

Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Katiba ya Syria kutoka upande wa Serikali Ahmad Kuzbari, amesema mchakato huo utafanikiwa pindi kila upande utakuwa na nia njema kwa maslahi ya nchi yao.

"Inazingatiwa kuwa ni mchakato wa kisiasa wa kumaliza mzozo ambao umeharibu nchi yetu. Mchakato huu unaweza kufanikiwa kwa dhamira thabiti na uamuzi dhahiri wenye imani njema pamoja na kufanya bidii kuhifadhi umoja, na uhuru wa nchi yetu. Kuhakikisha haki za watu wetu na ujasiri na nguvu ya nchi yetu," amesema Kuzbari.

Lakini wataalamu wanahoji iwapo serikali ya Rais Bashar al-Assad itakuwa tayari kukubali mengi yatakayojadiliwa katika mezi ya mazungumzo baada ya jeshi lake kuchukua udhibiti mkubwa wa ardhi nchini humo.

Syrien Ras Al Ayn Türkische Armee
Viksoi vya jashi la Uturuki katika mji wa mpakani wa Ras al-Ayn kaskazini mwa SyriaPicha: picture-alliance/AA/Turkish Armed Forces

Washirika wana matumaini

Urusi na Iran, washirika wa serikali ya Syria pamoja na Uturuki inayounga mkono upande wa upinzani, wanauangalia mkutano huo wa Kamati ya Katiba kama fursa ya kujenga imani miongoni mwa pande zote na kusaficha njia kuelekea mchakato mpana zaidi wa kisiasa ambao utaweza kumaliza mgogoro huo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov amezihimiza pande zote husika kufikia makubaliano.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema nchi hizo washirika hazitoingilia mchakato huo, na mwenzake wa Uturuki Mevlut Cavusoglu amesema ana matumaini lakini pia anafahamu kuwa mazungumzo hayo yatakuwa magumu.

Wakati huo huo, televisheni ya taifa ya Syria imeripoti juu ya mapigano makali kati ya vikosi vya serikali ya Syria na vya Uturuki katika eneo la mpakani la Ras al-Ayn, wakati ambapo rais wa uturuki Reccep Tayyip Erdogan akitangaza kuanza kwa doria ya pamoja kati ya vikosi vya Uturuki na Urusi kaskazini-mashariki mwa Syria.

rtre, dpa