1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Palmyra yarudi tena mikononi mwa IS

12 Desemba 2016

Wakati vikosi vya serikali vikiyachukuwa maeneo ya mashariki mwa Aleppo na Marekani na Urusi zikipendekeza mpango wa msamaha kwa waasi, kundi linalojiita Dola la Kiislamu (IS) limeurejesha mji wa Palmyra mikononi mwake.

https://p.dw.com/p/2U7U6
Syrien Zivilisten verlassen den Osten von Aleppo
Picha: Getty Images/AFP/G. Ourfalian

Kwa mujibu wa Shirika la Haki za Binaadamu la Syria lenye makao yake London, Uingereza, licha ya kuendelea kwa mashambulizi ya anga yanayofanywa na jeshi la Urusi, wapiganaji wa IS wamefanikiwa kuuchukuwa tena mji wote wa Palmyra.

Hapo jana, wapiganaji wa IS waliondoka Palymra, lakini hivi leo shirika la habari la Amaq, lenye mafungamano na kundi hilo, limeripoti kuwa mji huo wa kale uko mikononi mwao. 

Kwa mujibu wa mashirika yanayofuatilia vita vya Syria, wapiganaji wa IS walijikusanya nje ya mji na kuanzisha kampeni kubwa ya kuutwaa tena mji huo muhimu na wakafanikiwa. 

Kwa hatua hii, sasa majengo na masanamu ya kale yaliyosalia kwenye mji huo ulio kwenye Turathi za Umoja wa Mataifa, yako hatarini kumalizwa. IS wanayachukulia baadhi ya majengo na masanamu hayo kuwa ni kufuru dhidi ya Uislamu, na wamekuwa wakiyavunja kupinga kile wanachokiita "shirki".

Hayo yakiendelea, kwenye mapambano ya kulitwaa eneo la mashariki mwa Aleppo, Marekani na Urusi zinaripotiwa kutoa mapendekezo kwa waasi, ambayo yatawaruhusu wapiganaji kuondoka kwenye mji huo, wakiwa na familia zao na raia wengine. 

Makundi matatu ya waasi yameliambia shirika la habari la Reuters kuwa mapendekezo hayo yanatoa ahadi ya uondokaji wa salama na wa heshima, ingawa hadi sasa haijakuwa wazi kama watayakubali. 

Waasi zaidi ya 700, raia zaidi ya 13,000 waondoka mashariki mwa Aleppo

Syrien Oasenstadt Palmyra
Wapiganaji wanaojiita Dola la Kiislamu (IS) huwa wanayabomoa majengo ya kale ya Palmyra kwa madai ya kutumiwa kwa ibada za kishirikina.Picha: picture-alliance/dpa/V. Sharifulin

Awali Urusi ilikuwa imekanusha kuwepo makubaliano yoyote, ikisema kuwa ripoti za kuwepo kwa "mapendekezo hayo haziendani na ukweli wa mambo". 

Hata hivyo, baadaye wizara yake ya ulinzi ilisema kuwa waasi 728 wameweka chini silaha zao ndani ya kipindi cha masaa 24 yaliyopita na kuhamishiwa magharibi mwa Aleppo, katika eneo linalodhibitiwa na serikali.

Vile vile, kwa mujibu wa Urusi, raia 13,346 wameshaondoka kwenye upande wa mashariki mwa Aleppo ndani ya kipindi hicho hicho.

Badala yake, ripoti za hivi karibuni zinaelezea kuendelea kwa mashambulizi makali ya anga na ardhini kutoka ndege za Urusi na vikosi vya serikali. 

Mwandishi wa Reuters kwenye eneo hilo anasema usiku wa kuamkia leo ulikuwa na mashambulizi makubwa kabisa kuwahi kutokea.

Shirika la Haki za Binaadamu la Syria linasema kuwa asubuhi ya leo, vikosi vya serikali vilikitwaa kitongoji chengine cha Sheikh Saeed kutoka kwa waasi, hiyo ikimaanisha kuwa sasa waasi wameshapoteza asilimia 90 ya maeneo yao.

Marekani na Urusi zimekuwa zikifanya mazungumzo mjini Geneva, kusaka njia za kusimamisha mapigano na kushughulikia hali mbaya ya kibinaadamu iliyoko huko. 

Raia 413 wameuawa mashariki mwa Aleppo tangu kuanza kwa operesheni ya Urusi na Syria tarehe 15 Novemba, huku waasi wakiwauwa watu 139 upande wa magharibi.

Kwa ujumla, vita vya Syria vilivyoanza Machi 2011, vimekwishayaangamiza maisha ya watu wapatao laki tatu hadi sasa.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Daniel Gakuba