Ouattara ashinda muhula wa tatu Cote d'Ivoire kwa kishindo
3 Novemba 2020Tume ya uchaguzi ya Ivory Coast imetangaza Alassane Outtara kama mshindi wa uchaguzi, aliyepata ushindi wa kishindo wa asilimia 94.27 ya kura zilizopigwa. Wakati anamtangaza mshindi wa uchaguzi huo leo Jumanne asubuhi, Rais wa tume hiyo huru ya uchaguzi, Ibrahime Coulibaly-Kuibert, alisema: Watu waliojitokeza kupiga kura walikuwa ni asilimia 53.90 na Alassane Ouattara amepata kura milioni 3,031,483 kati ya kura zote zilizopigwa. Hiyo ni sawa na asilimia 94.27. Hiyo inamaanisha Rais mteule wa Jamhuri ni bwana Alassane Ouatara.
Soma pia: Ouattara ashinda uchaguzi huku wakiuonya upinzani
Watu waliojitokeza kupiga kura katika uchaguzi huo uliofanyika siku ya Jumamosi ya tarehe 31 Oktoba, walikua ni asilimia 53.90 ya wapiga kura wote. Matokeo hayo ya uchaguzi yanasubiri kuhalalishwa na baraza la katiba ya nchi hiyo. Kwa sasa kuna kipindi kifupi cha kusubiri kama kuna changamoto au malalamiko yoyote yatakayojitokeza.
Wapinzani wawili wakuu wa uchaguzi huo waliwaambia wafuasi wao wasiende kupiga kura katika uchaguzi huo wa Jumamosi kama njia ya kupinga kitendo cha Ouattara kugombea kwa muhula wa tatu. Wanaharakati wa upinzani wanaamini kwamba kitendo hicho cha bwana Outtara kugombea muhula wa tatu kinaenda kinyume na matakwa ya kidemokrasia.
Ouattara mwenye miaka 78 alipata zaidi ya asilimia 90 ya kura katika mikoa mingi ya nchi hiyo, ingawa vyama vya upinzani vinasema kwamba mpango wake wa kubakia madarakani upo kinyume na sheria.
Katiba ya Ivory Coast inaweka ukomo wa kipindi cha Urais kwa mihula miwili, lakini Ouattara anasema marekebisho ya katiba ya mwaka 2016, yanamruhusu yeye kuanza upya mamlaka yake ya Urais.
Soma pia: Cote d'Ivoire yaahidi uchaguzi huru na wa haki
Uchaguzi huo ulikumbwa pia na machafuko ya kabla ya uchaguzi kupelekea mauji ya watu takribani 30 huku kukiwa kuna hofu kwamba machafuko na migogoro yatajirudia kama ilivyotokea mwaka 2010 mpaka 2011.
Machafuko ya kipindi hicho yalipelekea mauaji ya takribani watu 3000 na yalisababishwa na Rais wa kipindi hicho, Laurent Gbagbo, kutotaka kukubali matokeo ya kushindwa uchaguzi.
Harrison Mwilima
Reuters