Orodha ya wapinzani yakwaza mialiko kwa mazungumzo ya Syria
19 Januari 2016Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amezitaka nchi kubwa duniani kukubaliana haraka juu ya makundi ya wapinzani yatakayohudhuria ili mazungumzo yaanze kama ilivyopangwa. Wito wa Katibu Mkuu Ban Ki-moon umetolewa wakati mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria Staffan de Mistura alipolihutubia Baraza la Usalama la Umoja huo kwa njia ya video kuhusu juhudi zake za kuzikutanisha Urusi ambayo inaunga mkono serikali ya rais Bashar al-Assad ana Qatar ambayo inawasaidia wapinzani ili ziweze kupunguza tofauti zao kuhusu makundi yanayopaswa kuhudhuria mazungumzo hayo yanayopangwa kufanywa mjini Geneva Jumatatu ijayo.
Msemaji wa Ban Ki-moon, Farhan Haq amesema Umoja wa Mataifa unalenga kuyaitisha mazungumzo hayo kwa muda uliopangwa, lakini hauwezi kutuma mialiko hadi pale nchi muhimu zitakapoafikiana juu ya orodha ya wapinzani. Hata hivyo hakuondoa uwezekano kuwa muda huo ambao ni tarehe 25 mwezi huu wa Januari inaweza kubadilishwa kutokana na changamoto mbalimbali.
''Bila shaka bado kuna wasiwasi katika mipangilio, na hivi tunavyozungumza Katibu Mkuu anafanya mashauriano na wajumbe wa Baraza la Usalama. Tutaangalia kama wadau wote, likiwemo Baraza la Usalama wataafikiana juu ya namna ya kusonga mbele'' amesema msemaji huyo, na kuongeza kuwa ratiba itabadilika wadau watajulishwa.
Sauti moja kuunga mkono mazungumzo
Balozi wa Uruguay katika Umoja wa Mataifa Elbio Rosselli ambaye kwa sasa ndie rais wa Baraza la Usalama amesema nchi zote 15 wanachama wa baraza hilo zinaunga mkono kwa kauli moja juhudi za mjumbe wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria, akisisitiza kwamba hakuna tarehe nyingine ya mazungumzo inayofikiriwa.
Kauli yake imeungwa mkono na balozi wa Urusi Vitaly Churkin, ambaye amesema ingawa chocote kinawezekana kwa wakati huu, ilikuwa vyema zaidi kuendelea kuzingatia tarehe iliyokwishatangazwa.
Katika juhudi hizo hizo kuelekea mazungumzo ya Syria, Staffan de Mistura ameliambia Baraza la Usalama, kwamba amehakikishiwa na Saudi Arabia na Iran kwamba mzozo wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili hautaathiri maandalizi ya mazungumzo ya amani.
Kitisho cha IS chaleta muafaka
Sauti moja kutoka Baraza la Usalama ambalo kwa miaka minne limekuwa na mgawanyiko mkubwa kuhusu Syria, imetokana na utambuzi wa nchi kubwa duniani, kwamba kipaumbele kwa wakati huu ni kulishinda kundi linalojiita Dola la Kiislamu - IS, ambalo limetumia mzozo wa nchi hiyo kujiimarisha na kufanya mashambulizi ya umwagaji damu katika nchi za nje.
Balozi wa Urusi kwenye Umoja wa Mataifa amesema nchi yake inaamini kwamba ujumbe wa upinzani unapaswa kuwakilisha makundi mengi iwezekanavyo, akiongeza kuwa kutengwa kwa baadhi ya viongozi wa upinzani wanaofahamika sana hakutaleta tija.
Hakuna matumaini makubwa ya kupata haraka suluhisho kwa mzozo wa Syria, na ushindi wa hivi karibuni wa serikali ya nchi hiyo kwenye uwanja wa mapambano, unaweza kuufanya utawala wa rais Bashar al-Assad kutoona ulazima mkubwa wa kufanya mazungumzo na kujitolea kutafuta maridhiano.
Mwandishi: Daniel Gakuba/ape/dpae/afpe
Mhariri: Grace Patricia Kabogo