Ongezeko la maambukizi ya Corona latia hofu Ujerumani
8 Oktoba 2020Lothar Wieler, mkuu wa taasisi ya udhibiti wa magonjwa ya Robert Koch , ameonya kwamba Ujerumani inaweza kushuhudia usambaaji ambao hautaweza kudhibitiwa wa virusi vya corona. Nchi hiyo yenye uchumi mkubwa barani Ulaya ilirekodi maambukizo mapya ya COVID-19 , 4,058 katika muda wa masaa 24, ikiwa ni ongezeko kubwa katika idadi iliyotolewa jana ya watu 2,828, kwa mujibu wa Taasisi ya Robert Koch.
"Tarakimu hizo zinaonesha ongezeko linalotia hofu ," Spahn waziri wa afya wa Ujerumani aliwaambia waandishi habari mjini Berlin, na kuwataka Wajerumani kutopuuzia hatua za kuzuwia usambaaji wa virusi hivyo hatari.
"Hakuna nchi nyingi barani Ulaya ambazo zimeweza kupambana na mzozo huo pia hadi sasa," amesema. "Lakini hatuwezi kuchukulia kama mchezo wa kamari kile ambacho tumefanikiwa hadi sasa."
Ongezeko hilo la maambukizo linalotia hofu limekuja wakati wa likizo za shule katika majira haya ya mapukutiko zikianza ama zikiendelea nchini Ujerumani, na kusababisha miito kutoka katika serikali ya kansela Angela Merkel kwa raia kuepuka kusafiri nje ya nchi wakati huu wa kipindi chenye shughuli nyingi kwa ajili ya utalii.
Majimbo yaimarisha sheria kuhusu virusi vya corona
Majimbo 16 ya Ujerumani pia yameimarisha sheria kwa ajili ya safari za ndani, ambapo wengi wakikubaliana na marufuku ya kukaa katika mahoteli, ama nyumba za kukodi wakati wa likizo kwa wasafiri kutoka katika maeneo yanayofahamika kama yenye hatari nchini humo.
Serikali ya Uingereza inatafakari kuweka vizuwizi vipya katika maisha ya kila siku nchini Uingereza huku kukiwa na ushahidi kuwa hatua hadi sasa hazijaleta mafanikio ya kutosha kuzuwia maambukizi mapya ya virusi vya corona. Wakati idadi ya watu wanaohitaji kwenda hospitali wakiwa na dalili zinazoelekea kuwa na maambukizo ya virusi vya corona ikiongezeka, na katika baadhi ya maeneo kaskazini mwa Uingereza hali ikiwa ni mbaya, shinikizo dhidi ya serikali kuchukua hatua zaidi linaongezeka pia.
Kampuni ya Gilead Sciences imesema leo kuwa imekubali kuiuzia ulaya hadi dozi 500,000 la dawa ya remdesivir, wakati bara la Ulaya linahangaika kuongeza upatikanaji wa dawa hiyo ambayo ni moja kati ya dawa aina mbili zilizothibitishwa hadi sasa kutibu wagonjwa wa COVID-19. Makubaliano hayo yanajumuisha ununuzi wa dawa hiyo kwa miezi sita ijayo kwa mataifa 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya , Uingereza, mataifa sita ya eneo la balkan pamoja na Iceland, Liechtenstein na Norway.