1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama kwa Wademocrat: "Tuingie kazini sasa"

21 Agosti 2024

Rais wa zamani wa Marekani Barack Obama amerudi katika jukwaa la kitaifa usiku wa kuamkia Jumatano ili kumuunga mkono Kamala Harris katika azma yake ya kuwania urais dhidi ya Donald Trump.

https://p.dw.com/p/4jiFk
Rais wa zamani wa Marekani Barack Obama
Rais wa zamani wa Marekani Barack ObamaPicha: Charly Triballeau/AFP/Getty Images

Wakiwatahadharisha Wademocrat kwamba wana mapambano makali mbele yao, rais wa zamani wa Marekani Barack Obama na mkewe Michelle, Jumanne, walitoa wito kwa Wamarekani kumkumbatia Kamala Harris katika ujumbe walioutoa katika Mkutano Mkuu wa Chama cha Democratic huko Chicago.

"Marekani, matumaini yanarudi," alisema Michelle Obama. Baada ya hapo bi Obama akamshambulia Donald Trump, kinyume na ilivyokuwa katika hotuba yake ya mkutano mkuu wa chama hicho mwaka 2016 aliposema, "wakienda chini, tunainuka."

Michelle Obama akiuhutubia Mkutano Mkuu wa Chama cha Democratic
Michelle Obama akiuhutubia Mkutano Mkuu wa Chama cha DemocraticPicha: Eva Hambach/AFP/Getty Images

"Mtazamo wake mdogo na mwembamba wa ulimwengu ulimfanya atishike na uwepo wa watu wawili wachapa kazi, walio na elimu ya juu, waliofanikiwa na ambao walikuwa weusi," alisema Obama kumhusu Trump.

Rais huyo wa zamani, alimuita Trump, "bilionea mwenye umri wa miaka 78 ambaye hajaacha kulalamikia matatizo yake." Obama alisema kwamba hali hiyo ya Trump kwa sasa imezidi kwa kuwa anaelekea kushindwa na Kamala Harris.

Obama alihitimisha hotuba yake kwa kuwaambia Wademocrat, "tuingie kazini."

Watu maarufu na hata Warepublican wajiunga na kampeni ya Harris

Ujumbe huo uliotolewa na Obama na mkewe umeonyesha dharura iliyoko wakati ambapo Harris anafanya juhudi za kuunda muungano mpana katika azma yake ya kumshinda Trump katika uchaguzi utakaofanyika katika msimu wa mapukutiko.

Harris anawaita watu nyota kujiunga na kampeni yake kama Obama na mkewe na watu wengine maarufu, maafisa kutoka mirengo ya kushoto, ya kati na hata baadhi ya Warepublican ili kuitia nguvu kampeni yake.

Kabla hotuba ya Obama na mkewe, Kamala Harris, aliuhutubia umati uliokadiriwa kuwa wa watu 15,000 katika jimbo la Wisconsin alipokuwa akifanya kampeni, katika ukumbi ule ule alioteuliwa Donald Trump kama mgombea wa urais wa chama cha Republican katika mkutano mkuu wa chama hicho mwezi Julai.

Kamala Harris akiwa Wisconsin katika mkutano wa kampeni
Kamala Harris akiwa Wisconsin katika mkutano wa kampeniPicha: Anna Moneymaker/Getty Images

Harris alisema kwamba "anafanya kampeni inayotiwa nguvu na watu."

"Kwa pamoja tutapata njia mpya ya mustakabali wetu, mustakabali wa uhuru, fursa, matumaini na imani," alisema makamu huyo wa rais, katika sehemu ya hotuba iliyorushwa katika mkutano mkuu wa Democratic huko Chicago.

Wengine waliotoa hotuba huko Chicago ni Seneta Chuck Schumer ambaye ndiye kiongozi wa wengi katika bunge la seneti na Bernie Sanders ambao wote walimmiminia sifa Harris.

Warepublican wamuasi Trump

Na katika kile ambacho labda kinatarajiwa kimtekenye Trump, msemaji wake wa zamani katika ikulu ya White House ambaye kwa sasa ni mkosoaji mkubwa wa huyo mkuu wake wa zamani, Stephanie Grisham, pia alipanda jukwaani na kutoa hotuba.

Msemaji wa zamani wa Trump katika White House Stephanie Grisham
Msemaji wa zamani wa Trump katika White House Stephanie GrishamPicha: RW/MediaPunch/picture alliance

"Trump hana huruma, hana tabia njema na si mkweli," alisema Grisham. "Naipenda nchi yangu zaidi ya chama changu(Republican). Kamala Harris anasema ukweli. Anawaheshimu Wamarekani. Na nitampigia kura."

Warepublican wengine ambao wamekiasi chama cha Republican tangu Trump aidhinishwe kama mgombea wao, walitoa hotuba pia katika mkutano huo mkuu wa chama cha Democratic.

Walizungumzia kitisho kinachoikabili demokrasia ya Marekani iwapo Trump atashinda uchaguzi wa Novemba 5.

Wapiga kura Wahafidhina wasiompenda Trump wamekuwa mojawapo ya matumaini ya Wademocrat ila changamoto itakuwa kuwashawishi wampigie kura Harris mwezi Novemba badala ya kusalia majumbani.

Chanzo: DW/Reuters/APE