Obama haoni uwezekano wa kupeleka jeshi Syria
4 Mei 2013"Kama sheria ilivyo kwa jumla , siondoi uwezekano , kama mkuu wa majeshi kwasababu hali inabadilika na unataka kuhakikisha kuwa kila wakati nguvu za Marekani zinakuwapo kuweza kutimiza maslahi ya taifa ya kiusalama, " amesema Obama.
"Baada ya kusema hayo, siioni hali kwamba wanajeshi wa Marekani wataingia katika ardhi ya Syria , wanajeshi wa marekani nchini Syria , hawataleta manufaa kwa Marekani tu , lakini pia wataleta manufaa kwa Syria."
Uvumi umekuwa ukiongezeka kuwa utawala wa rais Obama unaweza kubadilisha upinzani wake wa kuwapa silaha waasi baada ya Ikulu ya nchi hiyo kusema wiki iliyopita kuwa rais Bashar al Assad huenda alitumia silaha za kemikali dhidi ya watu wake.
Msitari mwekundu
Obama amekuwa akijizuwia kuingilia kati katika vita lakini anakabiliwa na ukosoaji kuwa ameruhusu utawala wa Assad kuvuka msitari mwekundu alioutangaza, iwapo zitatumika silaha za kemikali.
Lakini rais huyo wa Marekani pia amesisitiza kuwa ushahidi zaidi unahitajika kwa nchi hiyo kuchukua hatua kujihusisha katika vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo tayari vimesababisha vifo vya zaidi ya watu 70,000 , na hivi sasa mzozo huo unaingia katika mwaka wa tatu.
Akizungumza wakati wa ziara yake nchini Costa rica , Obama amesema kuwa kuna ushahidi kuwa silaha za kemikali zimetumika nchini Syria, lakini ni kwamba "hatufahamu ni lini, wapi ama vipi zilitumika."
"Lakini amedokeza kuwa ushahidi wowote imara kwamba utawala wa Assad ulitumia silaha hizo utabadilisha utaratibu wa mchezo", kwa sababu silaha hizo zinaweza kuangukia katika mikono ya makundi kama kundi la wanamgambo wa Hezbollah , lililoko katika nchi jirani ya Lebanon.
"Kwa misingi ya hatua zozote za ziada ambazo tutachukua, zitakuwa katika msingi, wa kwanza ushahidi kuhusiana na kilichotokea , tena itahusiana na kile ambacho kitakuwa kwa maslahi ya watu wa Marekani na usalama wa taifa letu," ameongeza Obama.
"Kama rais wa Marekani nitafanya maamuzi hayo kwa misingi ya ushahidi sahihi na baada ya kushauriana kwa makini kwasababu iwapo tutaharakisha kufanya jambo, iwapo jutachupa kabla ya kuangalia, basi sio kwamba sisi tutaathirika lakini mara nyingi, tumeona kunatokea mambo ambayo hayakutarajiwa katika hali kama hiyo.
Ulinzi wa silaha za kemikali
Wataalamu wanasema ujumbe wa kijeshi wa kwenda kuzilinda silaha hizo za kemikali utahitaji jeshi kubwa ardhini na hiyo italeta matatizo makubwa, ambapo matokeo yatategemea uwezo wa kijasusi wa mataifa ya magharibi.
Mkuu wa zamani wa wizara ya ulinzi Leon Panetta , ambaye alijiuzulu wadhifa wake Februari mwaka huu , aliwaambia wabunge kuwa yeye pamoja na maafisa wa ngazi ya juu wa jeshi la Marekani, Jenerali Martin Dempsey, ameshauri waasi wapewe silaha lakini ushauri huo ulitenguliwa.
Nchini Syria wakati huo huo , majeshi ya serikali yameshambulia kwa mabomu maeneo ya Wasunni katika mji ulioko katika ukingoni mwa bahari ya Mediterranean wa Banias, kundi linalofanya uangalizi limesema , likionya kuhusu mauaji mapya ambapo yalisababisha watu 50 kuuwawa.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Sudi Mnette