Obama ahudhuria mkutano wa nchi za Asia Mashariki
20 Novemba 2012Rais wa Marekani Barack Obama amesema uhusiano kati ya nchi yake na China ni wa ushirikiano na wa maana. Amesema kuna umuhimu mkubwa kwa mataifa hayo mawili kushirikiana kuweka msingi wa sheria ulio wazi kwa ajili ya biashara na uwekezaji.
Kwa niaba ya utawala wa China unaoondoka na ule unaojiandaa kuchukua hatamu za uongozi, Wen amempongeza Obama kwa kuchaguliwa tena kuingoza Marekani. Mkutano huo ni wa mwisho kati ya Obama na Wen ambaye anaachia ngazi pamoja na rais wa China Hu Jintao katika mageuzi ya utawala katika kipindi cha muongo mmoja.
Wakati huo huo, rais Obama amefanya mazungumzo pia na waziri mkuu wa Japan, Yoshika Noda, pembezoni mwa mkutano huo. Noda ameonya kuhusu ongezeko la wasiwasi wa kiusalama barani Asia huku kukiwa na mivutano juu ya mipaka. Kiongozi huyo wa Japan anayetarajiwa kushindwa katika uchaguzi mwezi ujao, ameipongeza sera ya kigeni ya Obama kuelekea eneo hilo, akisema uhusiano kati ya Marekani na Japan ni muhimu kuzingatia hali ya usalama mashariki mwa Asia.
Obama akabiliwa na kibarua kigumu
Rais Obama anatarajiwa leo kupiga mbizi katika maji marefu ya kidiplomasia atakapozungumzia mzozo wa bahari ya China kusini. Anatarajiwa pia kuelezea wasiwasi wake kuhusu mzozo kati ya China na majirani zake wa kusini mashariki mwa Asia, ambao umezua wasiwasi katika eneo hilo mwaka huu na kukwamisha juhudi za kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi. Akizungumza hapo jana, Wen alisisitiza kwamba mzozo huo hautakiwi kufanywa kuwa wa kimataifa na kujadiliwa kwenye mikutano mikubwa kama wa Phnom Penh.
China, ambayo inadai bahari yote ni himaya yake, inapendelea kufanya mashauriano ya moja kwa moja na majirani zake kutoka Jumuiya ya mataifa ya kusini mashariki mwa Asia, ASEAN, wenye wanachama 10. Rais Obama amesema anaamini kuna haja ya kupunguza wasiwasi kuhusiana na mzozo wa mipaka katika bahari ya China
Lakini kwa mujibu wa taarifa ya mwisho ya mkutano wa jana kati ya Marekani na jumuiya ya ASEAN, Obama na viongozi wa jumuiya hiyo walikubaliana kuunga mkono muongozo wa sheria wa kanda hiyo kusuluhisha mivutano juu ya mipaka.
Cambodia ni kituo cha mwisho cha ziara ya siku tatu ya Obama kusini mashariki mwa Asia baada ya kuzitembelea Myanmar na Thailand.
Mwandishi: Josephat Charo/APE/AFPE/
Mhariri: Daniel Gakuba