Mabalozi wa UN wapiga hatua ndogo kuhusu mzozo wa Burundi
23 Januari 2016Mabalozi hao walikutana na Nkurunziza katika Ikulu ya Rais nje ya mji mkuu wa nchi hiyo na kumtolea wito wa kuchukua hatua za dharura kukomesha ghasia zilizochochewa na yeye kusalia madarakani kwa muhula wa tatu.
Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Samantha Power amesema hawakufanikiwa kama walivyotarajia katika mazungumzo yao.
Power ameongeza kusema kuna wito kutoka kwa raia wengi wa Burundi wa kupatikana masaada kutoka nje na kuchukuliwa kwa kwa juhudi za dharura za upatanishi ili kuupatia ufumbuzi mzozo huo uliozuka mwezi Aprili mwaka jana.
Nkurunziza asema Burundi ni salama
Nkurunziza amekatalia mbali wito wa kufanya mazungumzo na upinzani, kufufuliwa kwa juhudi za upatanishi na kupelekwa kwa kikosi cha wanajeshi 5,000 wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika nchini humo ili kurejesha uthabiti na badala yake ameishutumu nchi jirani ya Rwanda kwa kuyaunga mkono makundi ya waasi.
Nkurunziza amepuuzilia mbali hofu kuwa huenda kukatokea mauaji ya halaiki nchini humo na kusema Burundi iko salama kwa asilimia 99. Mabalozi hao leo Jumamosi (23.01.2016) watafanya mazungumzo na viongozi wa Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa, Ethiopia kuhusu mzozo huo wa Burundi.
Nchi hiyo imekumbwa na ghasia tangu Nkurunziza kutangaza kugombea muhula wa tatu madarakani kinyume na katiba ya nchi hiyo.
Zaidi ya watu 400 wameuawa tangu mzozo huo kuzuka huku wengine zaidi ya laki mbili wametorokea nchi jirani. Serikali ya Burundi imesisitiza hakuna haja ya wanajeshi wa kigeni na kulitaja pendekezo la kupelekwa wanajeshi wa Umoja wa Afrika kama uvamizi.
Uhusiano kati ya Burundi na Rwanda uko tete kutokana na utawala wa Nkurunziza kuishutumi nchi hiyo jirani kwa kuyaunga mkono makundi ya waasi na wanasiasa wanaompinga Nkurunziza. Rwanda imekanusha madai hayo.
Msimamo mkali wa Nkurunziza wa kukataa kufanya mazungumzo na wapinzani wake, kutumwa wanajeshi wa kigeni na kuzipa nafasi juhudi za upatanishi kunatarajiwa kuchukuliwa kwa hatua kali kutoka kwa jumuiya ya kimataifa inayojaribu kuhakikisha taifa hilo halitumbukii katika vita vya wenyewe vitakavyosababisha mauaji ya halaiki.
Kipi kitafuata?
Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Afrika Nkosazana Dlamini Zuma alikuwa ameelezea imani yake kubwa kuwa wajumbe hao wa Baraza la Umoja wa Mataifa watasaidia katika kuishurutisha serikali ya Burundi kukubali kupelekwa kwa wanajeshi wa kulinda amani na kurejea katika meza ya mazungumzo na wapinzani.
Marekani na Ufaransa wanaunga mkono mapendekezo ya Umoja wa Afrika lakini nchi wanachama wengine wa Baraza hilo kama Urusi, Angola na Misri wanasita kuiwekea mbinyo zaidi serikali ya Burundi.
Ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa pia ulikutana na marais wa zamani wa Burundi, viongozi wa asasi za kiraia, viongozi wa kidini na viongozi wa vyombo vya habari.
Siku ya Alhamisi, marais wawili wa zamani wa Burundi Jean Baptiste Bagaza na Domitien Ndayizeye waliwaomba mabalozi hao wa Umoja wa Mataifa kuchukua hatua kukomesha ghasia nchini humo na kushinikiza kupelekwa kwa wanajeshi wa kulinda amani.
Umoja wa Afrika utafanya mkutano wa kilele kati ya tarehe 30 na 31 mwezi huu wa Januari na mzozo huo wa Burundi ukitarajiwa kupewa kipaumbele katika mazungumzo ya mkutano huo.
Mwandishi: Caro Robi/afp/Reuters
Mhariri: Sekione Kitojo