Nigeria yadhinisha chanjo ya Malaria ya Chuo cha Oxford
18 Aprili 2023Nigeria imetoa idhini ya muda ya chanjo ya Malaria ya R21 ya Chuo Kikuu cha Oxford. Hatua hiyo inaifanya Nigeria kuwa nchi ya pili baada ya Ghana kuidhinisha matumizi ya chanjo ya Malaria wiki iliyopita. Uidhinishaji huo usio wa kawaida umefanyika kabla ya uchapishaji wa data wa hatua ya mwisho ya majaribio ya chanjo.
Mamlaka ya taifa ya usimamizi wa chakula na dawa ya Nigeria NAFDAC imesema katika taarifa yake kwamba uidhinishaji huo wa muda utatumika kwa kuzingatia mwongozo wa utekelezaji chanjo wa shirika la afya ulimwenguni WHO.
Malaria, ugonjwa unaoenezwa na mbu unaua zaidi ya watu laki 600,000 kila mwaka, wengi wao wakiwa watoto wachanga wa Afrika. Nigeria nchi yenye watu wengi barani Afrika ndio imeathirika zaidi ikiwa na asilimia 27 ya visa na asilimia 32 ya vifo vya Malaria duniani kote.