Niger yaidhinisha wanajeshi wa Mali na Burkina Faso
25 Agosti 2023Viongozi wa kijeshi wa Niger wameidhinisha vikosi vya Mali na Burkina Faso kuingia katika ardhi yake endapo nchi hiyo itashambuliwa. Taarifa hiyo ya pamoja iliyotolewa na nchi hizo tatu inaashiria kwamba viongozi wa mapinduzi wa Niger wanapanga kuendelea kukataa shinikizo la kikanda la kuachia madaraka.
Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi hizo tatu walikutana mjini Niamey jana ili kujadili ushirikiano zaidi wa kiusalama na masuala mengine. Burkina Faso na Mali zimekariri msimamo wao wa kukataa uingiliaji wowote wa kijeshi dhidi ya Niger ukiutaja kama tangazo la vita.
Jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi ECOWAS, imekuwa ikijaribu kufanya majadiliano na viongozi wa mapinduzi lakini imeonya kwamba iko tayari kupeleka wanajeshi nchini humo kwa lengo la kurejesha utulivu ikiwa juhudi za diplomasia zitashindikana.