Ni miaka 25 tangu kuanguka Ukuta wa Berlin
7 Novemba 2014Kuanguka Ukuta wa Berlin kulipelekea miezi 11 badae kuungana upya Ujerumani. Walikuwa wabunge waliofungua rasmi sherehe hizo leo asubuhi katika jengo la Reichtag mjini Berlin.Wakuu wa makundi tofauti ya bunge la shirikisho Bundestag walipanda jukwaani na kuelezea kumbu kumbu zao kuhusiana na tukio hilo la kihistoria. Wageni wasiopungua milioni mbili wanatarajiwa kushiriki katika sherehe zinazoanza leo hii mjini Berlin.
Leo usiku mabofu elfu nane yaliyofungwa kama mnyonyoro yatamulika mahala ukuta huo huo ulikopita kabla ya kurushwa hewani jumapili ijayo saa za usiku yakisindikizwa na wimbo wa Ludwig von Beethoven Ode of Joy au "Utenzi wa Furaha" ambao ndio uliochaguliwa kuwa wimbo wa Umoja wa Ulaya.
Sambamba na hayo Michael Gorbatchov,mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel mwenye umri wa miaka 83 hivi sasa,atafika pia ziarani mjini Berlin anakojivunia umashuhuri mkubwa kuliko hata nchini mwake Urusi,akishukuriwa kwa mchango wake katika kuziunganisha upya Ujerumani mbili.
Kesho kiongozi huyo wa mwisho wa enzi ya Usovieti atashiriki katika mjadala pamoja na waziri wa zamani wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Hans Dietrich Gensccher kuzungumzia kuzuka upya hali ya mvutano kati ya nchi za magharibi na Urusi.Na jumatatu usiku Mikhael Gorbatchov amepangiwa kuzungumza na kansela Angela Merkel.
"Ukuta wa aibu" kama ulivyokuwa ukiitwa na nchi za magharibi au ukuta wa kinga dhidi ya ufashisti" kama ulivyokuwa ukiitiwa na kambi ya mashariki ulijengwa na jamhuri ya kidemokrasia ya mashariki au GDR mwaka 1961 na ulienea zaidi ya kilomita 150.Ukiangukia mhanga wa siasa ya uwazi ya rais wa Usovieti Michael Gorbatchov na shinikizo la malaki ya wajerumani masdhariki wliokuwa wakiandmna kwa amani,ukuta huo uliporomoka,miaka 28 baadae,novemba 9 mwaka 1989.Chini ya mwaka mmoja baadae,octoba tatu mwaka 1990 Ujerumani zikaungana upya.
Kansela Angela Merkel aliyekuliwa GDR na mwaka 1989 akiishi Berlin Mashariki alifichua hivi karibuni "hisia zisizoelezeka"alizokuwa nazo Novemba 9 mwaka 1989,atafungua jumapili asubuhi maonyesho mepya katika makumbusho ya Ukuta wa Berlin na kuhudhuria burudani katika ukumbi mashuhuri wa jiji la Berlin.
Jumapili pia lango la Brandenburg lililoko kati kati ya jiji la Berlin litageuka kitovu cha sherehe zilizopewa jina "Moyo wa uhuru" zitakazohudhuriwa na rais Joachim Gauck,rais wa zamani wa Usovieti Michael Gorbatchov,na rais wa zamani wa Poland,mpigania uhru Lech Walesa.
Wasanii mashuhuri tangu wa Ujerumani mpaka wa kimataifa ikiwa ni pamoja na Peter Gabriel wa Uingereza, aliyetunga nyimbo kuwasiifu mashujaa,nyimbo iliyoimbwa na David Bowie mwaka 1977 alipokuwa anaishi Berlin Magharibi,watawatumbuiza washiriki wa sherehe hizo.
Wasanii wengine ikiwa ni pamoja na Udo Lindenberg wa Ujerumani aliyetunga nyimbo Treni kuelekea Pankow mwaka 1983 wanatarajiwa kuwatumbuiza washiriki jumapili usiku.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP
Mhariri:Yusuf Saumu