Nagelsmann asema ni mapema kujua mshindi wa ligi ya mabingwa
28 Septemba 2021Hii ni baada ya mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Ufaransa ambaye aliwahi kushinda kombe la dunia na lile la ulaya Robert Pires kuitaja Bayern Munich kama timu bora zaidi ulaya na inayotazamiwa kuwa italitwaa kombe hilo.
Bayern watawaalika nyumbani Allianz Arena Dynamo Kyiv Jumatano hii katika mechi ya pili ya kundi E katika mashindano ya Champions League.
" Kwanza kabisa, Pires alikua mchezaji mzuri sana, na pindi mchezaji mzuri anapotoa maoni, sina budi kuyasikiliza. Lakini kilicho muhimu wakati wote, ni lazima utoke nje na uthibitishe kile ambacho watu wanasema juu yako," alisema Nagelsmann katika mkutano kwa njia ya video na waandishi wa habari.
Bavaria kama wanavyojulikna kwa jina la utani na ambao walishinda mara ya mwisho ligi ya Mabingwa mnamo mwaka 2020, waliipa kichapo cha 3-0 Barcelona Uhispania katika mchezo wao wa ufunguzi na wameshinda michezo nane mfululizo katika mashindano yote.
Bayern pia inaongoza jedwali la Bundesliga.
" Yeyote anayetaka kushinda mashindano ya Ulaya kama vile ligi ya mabingwa lazima ashinde idadi kubwa zaidi ya mechi na tutajaribu kufanya hivyo. Kuna alama tatu zinazoweza kupatikana kesho, na tunataka kupata sita baada ya mechi mbili na kubaki kuwa wa kwanza katika kundi letu," alisema pia Nagelsmann.
Kocha huyo wa Bayern Munich atakuwa na kikosi kamili japo itazikosa huduma za kiungo Corentin Tolisso na Kingsley Coman, ambaye ameanza kupata afueni baada ya upasuaji mdogo wa moyo wiki mbili zilizopita.
Coman mwenye umri wa miaka 25 alionekana katika mazoezi na timu yake Jumatatu lakini bado hajawa tayari kurudi rasmi uwanjani.
Nagelsmann amesisitiza kuwa ili kuishinda Kyiv ni lazima kutafuta njia ya kupenya kwa kuwa Benfica walishindwa kuivunja ngome ya Kyiv japo amesisitiza kuwa ana imani na timu yake.