Ni kiasi gani cha maji unachohitaji mwili wetu?
4 Septemba 2023Karibu asilimia 80 ya mwili wa mtoto mchanga huundwa kwa maji. Tunapozeeka, kiwango cha maji katika mwili hupungua na kufikia karibu asilimia 60.
Seli za mafuta huwa na kiwango cha chini cha maji kuliko seli nyingine za mwili. Vivyo hivyo, watu walio na uzito kupindukia wana maji kidogo kuliko watu wembamba, na wanawake wana kiwango kidogo cha maji kuliko wanaume.
Kwetu sote hata hivyo, ni muhimu kwa maisha yetu kuupa maji mwili wetu mara kwa mara kwa kunywa.
Baadhi ya viungo huwa na kiasi kikubwa sana cha maji. Moja ya viungo hivyo ni jicho letu. Kioo chake kinaundwa na maji kwa hadi asilimia 99. Misuli pia ina kiwango cha juu cha maji kwa takriban asilimia 80.
Ili kuupa mwili wetu maji ya kutosha, tunaweza kufanya jambo moja zaidi ya yote: kunywa, kunywa na kunywa tena.
Kunywa maji siyo hiari
Mwili wetu hupoteza takriban lita mbili za maji kila siku, kwa upande mmoja kupitia ngozi, ambayo inadhibiti joto la mwili.
Hii ni kweli hasa katika hali ya hewa ya joto. Lakini hewa kavu ya joto inaweza pia kutuathiri.
Figo, ambazo huondoa sumu kwenye miili yetu, hutoa maji kwa namna ya mkojo. Ikiwa hatujakunywa vya kutosha, mkojo wetu una rangi ya manjano kali.
Ikiwa rangi yake ni kahawia, ni onyo kali kwamba kuna kitu kibaya.
Majimaji hutolewa kwenye kinyesi kupitia matumbo, na pia tunapoteza maji katika mfumo wa matone madogo tunapopumua.
Tunapaswa kufidia upotevu huu na hivyo tunywe lita 1.5 hadi mbili za maji kila siku.
Uhitaji huongezeka wakati wa mwili unaposhughulishwa, michezo, joto la juu, homa, kutapika na kuharisha. Hata hivyo sio lazima iwe maji kila wakati.
Supu, matunda au aina mbalimbali za mboga pia ni nzuri kwa mwili na kusaidia kujaza hifadhi.
Hii ni muhimu kabisa, kwa sababu mwili wetu tayari unaonyesha dalili za kwanza kwa kupoteza maji kwa asilimia moja hadi mbili.
Kuanzia upotezi wa karibu asilimia saba, tuko kwenye upande wa hatari: Mapigo ya haraka au kuchanganyikiwa huashiria hili, kwa sababu miitikio yote ya kemikali na taratibu katika mwili zinahitaji maji.
Kwa upungufu wa asilimia kumi na mbili, hali ya mshtuko au hata kuzimia kunaweza kutokea katika hali mbaya zaidi.
Ubongo wetu unahitaji maji ili kujilinda
Ubongo wetu na uti wa mgongo haviwezi kufanya kazi bila maji pia. Tuna takriban mililita 140 za maji ya neva au ubongo, kitabibu: ugiligili wa ubongo.
Ni umajimaji wa uwazi ambamo ubongo wetu huelea kwenye fuvu la kichwa na kuulinda dhidi ya mshtuko.
Kila siku tunazalisha karibu nusu lita ya maji haya, ambayo pia yanagawanywa tena na bila shaka yanahitaji kubadilishwa ipasavyo.
Ishara za kwanza kwamba mwili wetu unahitaji maji haraka ni maumivu ya kichwa na kizunguzungu, utando mkavu katika kinywa na koo, na uwezekano wa ugumu wa kumeza. Tumechoka na kuhisi wadhaifu, lakini mwanzoni hatuhusishi hii na ukosefu wa maji.
Kwa joto na upotezaji wa ziada wa maji kwa kutokwa na jasho, mzunguko wetu unaweza kushindwa na tunaweza kudhoofika.
Mwili unatuambia bila shaka ikiwani wakati wa haraka wa kunywa kitu, kwa sababu shinikizo la damu yetu pia linaongezeka.
Bila maji ya kutosha, damu yetu inakuwa nzito na haiwezi tena kudumisha mzunguko bila matatizo.
Kadiri unavyozeeka ndivyo unavyohisi kiu kidogo
Kadiri tunavyozeeka ndivyo tunavyohisi kiu kidogo. Pia ni jambo la kawaida kwa wazee kusahau tu kunywa vya kutosha.
Hii inaweza kusababisha kizunguzungu, kuchanganyikiwa, kupungua au kupoteza fahamu, miongoni mwa mambo mengine.
Katika hali ya upungufu mkubwa wa maji, madaktari wanapaswa kuupa kiwango kinachofaa kupitia unyweshaji.
Baadhi ya wazee, hata hivyo, kwa makusudi hujizuia kunywa vya kutosha, kwa sababu katika uzee wengi hawawezi tena kudhibiti mkojo pamoja na vijana.
Kwa hofu ya kutokwa na mkojo bila kukusudia au kulazimika kwenda choo mara nyingi sana usiku, wengi hunywa kidogo sana au kutokunywa kabisa.
Tunapohitaji maji mengi hasa
Ikiwa tunaharisha au kutapika, mwili wetu unahitaji zaidi ya kiwango cha chini cha lita 1.5 kwa siku. Ikiwa usawa wa maji haujarejeshwa haraka iwezekanavyo, mwili hukauka.
Kuchukua dawa fulani, kama vile za kuongeza mkojo, pia kunahitaji maji mengi. Zina athari ya kuongeza mkojo na hupunguza maji mwilini, kwa mfano, kuzuia edema, i.e. uhifadhi wa maji.
Pombe pia hufyonza mwili wetu kwa sababu ina athari ya kuongeza mkojo. Figo hujaribu kufuta vitu vya sumu kutoka mwilini, hivyo mara nyingi tunapaswa kwenda kwenye choo ili kutoa mkojo.
Pombe husababisha kutolewa kwa kinachojulikana kama vasopressin kwenye hypothalamus (kituo muhimu cha udhibiti wa mwili wetu kilichoko kwenye ubongo). Vasopressin ni homoni ambayo inasimamia usawa wa maji katika figo.
Hata hivyo, ikiwa mwili hauna homoni hii muhimu ya kutosha, figo zetu hutoa maji mengi. Uwiano wa maji unavurugika, kila kitu kinachanganyika.
Kunywa maji mengi inaweza kuwa hatari
Tukinywa lita tano au zaidi ndani ya masaa machache, hii inaweza pia kuwa hatari kwa maisha na kusababisha kinachojulikana kama hyperhydration, yaani maji yaliozidi mwilinii.
Hapo figo haziwezi tena kudhibiti na kutoa kiasi kikubwa cha maji. Moja ya matokeo mabaya zaidi inaweza kuwa edema ya ubongo.
Kiasi kikubwa cha kimimika humezwa wakati wa kunywa maji. Hii inaweza kuuchosha mwili.
Sio tu kwamba figo zinashindwa tena kufanya vyema kazi yake, usawa wa chumvi pia huharibiwa.
Namna na endapo mwili unaweza kukabiliana na maji mengi inategemea umri, uzito na hali ya jumla. Hapa, pia, ni kiasi kinachojalishwa.