Netanyahu yuko Washington kukutana na viongozi wa Marekani
24 Julai 2024Netanyahu alitarajiwa kukutana na Rais Joe Biden Jumanne. Hata hivyo, mkutano huo uliahirishwa hadi Alhamisikwa sababu rais anaendelea kupata nafuu baada ya kuambukizwa UVIKO-19. Ikulu ya White House imesema Makamu wa Rais Kamala Harris -- anayeongoza katika mbio za kupata uteuzi wa chama cha Democratic kwa uchaguzi wa rais Novemba mwaka huu - atakuwa na mkutano tofauti na kiongozi huyo wa Israel. Aidha anatarajiwa kukutana na mgombea wa urais Mrepublican Donald Trump Ijumaa.
Netanyahu pia atayahutubia mabaraza yote mawili ya Bunge la Congress leo Jumatano, kufuatia mwaliko kutoka kwa viongozi wa mabaraza hayo. Spika wa Baraza la Wawakilishi Mrepublican Mike Johnson angependa sana kuonesha uungaji mkono wake kwa Israel.
Soma pia: Vikosi vya Israel vyaendelea kuushambulia Ukanda wa Gaza
Licha ya uungaji mkono unaoendelea kuoneshwa na Marekani kwa operesheni za Israel huko Gaza, mahusuano kati ya Netanyahu na Biden yameharibika. Idadi ya vifo huko Gaza inaendelea kupanda, na kufikia zaidi ya watu 39,000, wengi wao raia, kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza inayoendeshwa na Hamas.