1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu kukutana na Merkel mjini Berlin

Admin.WagnerD21 Oktoba 2015

Waziri wa Mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry kuzungumza na Netanyahu Alhamisi. Mkutano huo unakuja wakati ghasia kati ya Wapalestina na Waisraeli zikiendelea.

https://p.dw.com/p/1GrNO
Angela Merkel und Benjamin Netanyahu
Picha: Getty Images

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, anatarajiwa kuwasili mjini Berlin Jumatano kwa mazungumzo na Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, huku ghasia zikipamba moto nchini Israel katika makabiliano na Wapalestina. Mazungumzo kati ya Waziri Mkuu Netanyahu na Kansela Merkel yatatuwama juu ya hali ya usalama inayokabiliana nayo Israel wakati huu pamoja na wasiwasi uliopo katika eneo la Mashariki ya Kati.

Mazungumzo ya viongozi hao wawili yatafanyika wakati wasiwasi ukizidi kutanda miongoni mwa raia nchini Israel, kufuatia mlolongo wa mashabulizi ya uchomaji visu yaliyofanywa na Wapalestina. Zaidi ya wapalestina 40, wakiwemo washambuliaji, wameuwawa katika mlolongo wa machafuko haya mapya yalioanza mwanzoni mwa mwezi huu. Waisraeli wanane wameuwawa katika mashambulizi hayo.

Kansela Merkel anaamini kwamba suluhisho la amani katika Mashariki ya Kati linahitaji kuwa chini ya zingatio la kuwepo kwa madola mawili yatakayoishi kwa ujirani, ikiwa na maana kuundwa kwa Dola ya Palestina, kandoni mwa taifa la Israel.

Wapalestina waandamana wakiwa wameshikilia visu
Wapalestina waandamana wakiwa wameshikilia visuPicha: Getty Images/AFP/M. Abed

Hata hivyo Kansela alishindwa katika mazungumzo yao yaliopita na Netanyahu, kumshawishi waziri mkuu huyo wa Israel kusitisha sera zenye utata za serikali yake juu ya kuendelea na ujenzi wa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi katika maeneo ya Wapalestina yanayokaliwa na Israel. kutokana na hayo suala hilo la makaazi linatarajiwa kuchukuwa nafasi ya usoni katika mazungumzo yao ya mjini Berlin, kabla ya Netanyahu kukutana na Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry mjini humo hapo Alhamisi.

Ban Ki-moon ataka amani irejee

Kerry anaondoka Washington kwa ziara hiyo ya ng'ambo katika jitihada za kutuliza machafuko yaliozuka kati ya Israel na Wapalestina, pamoja na kutathmini hatua za kuupa msukumo mpya mchakato wa amani nchini Syria. Kerry atakuweko Ulaya na Mashariki ya kati kwa muda wa siku tano, ziara ambayo mbali na kuzungumza na Waziri Mkuu Netanyahu wa Israel atakutana pia na Rais wa Palestina, Mahmoud Abbas na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi Sergei Lavrov.

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban-Ki-moon, ataliarifu Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu ziara yake ya Mashariki ya Kati, katika juhudi zakeb za kuituliza hali ya mambo. Ban alipendekeza kuzungumza na wanachama wa Baraza hilo kwa njia ya mawasiliano ya Video kutoka mji wa Wapalestina wa Ramadhallah kwenye Ukingo wa Magharibi. Katibu mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ameshakuwa na mazungumzo na Waziri mkuu wa Israel na atakutana na Rais wa Palestina.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman/dpa/ap/afp

Mhariri: Josephat Charo